Makamu mwenyekiti wa jukwaa la wahariri Theophil Makunga pamoja na wakili wa kujitegemea Juvenalis Ngowi wakimjulia hali Kibanda katika taasisi ya mifupa (MOI).
Wakati mhariri mtendaji wa kampuni ya New Habari Corparation, Absalom Kibanda akipelekwa nchini Afrika Kusini kwa ajili ya matibabu zaidi, chama cha waandishi wa habari za michezo Tanzania (TASWA) kimeungana na waandishi wa habari wote kulaani kitendo cha watu wasiojulikana kumvamia na kumjeruhi vibaya Kibanda.
Kibanda ambaye pia ni mwenyekiti wa jukwaa la wahariri, alikutwa na mkasa huo usiku wa kuamkia leo nyumbani kwake Mbezi Beach jijini Dar es salaam wakati akirejea kutoka kazini.
Kwa mujibu wa Ofisa Mtendaji Mkuu wa New Habari Corparation Hussein Bashe, wavamizi hao ambao hawakuiba wala kupora kitu chochote, walimjeruhi vibaya Kibanda sehemu za kichwani, huku pia wakimng'oa meno kadhaa, kumkata kidole na kumchoma na kitu chenye ncha kali jicho lake la kushoto.
Bashe alisema tukio hiyo ni la kusikitisha na halikupaswa kutokea kwani hakuna mwenye haki ya kumhukumu binadamu mwenzake.
Alisema kuwa pamoja na jitihada za madaktari wa Hospitali ya Taifa Muhimbili bado wameshauriwa kumpeleka Afrika Kusini kwa ajili ya uchunguzi zaidi katika jicho lake ambalo linaonekana kupata athari zaidi kuliko sehemu yeyote ya mwili wake.