Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mh. John Haule akielezea mafanikio mbalimbali ambayo Serikali ya Tanzania na Jamhuri ya Watu wa China zinajivunia kuyapata katika miaka 50 ya mahusiano ya kidiplomasia wakati akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) mapema hii leo jijini Dar es Salaam, kulia ni balozi wa China nchini Tanzania Mh. Dkt. Lu Youqing na kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari Assah Mwambene.
Balozi wa China nchini Tanzania Mh. Dkt. Lu Youqing (kulia) akifafanua mikakati ya nchi yake kuendelea kutoa mikopo nafuu kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali nchini Tanzania wakati akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) mapema hii leo jijini Dar es Salaam, kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mh. John Haule.Baadhi ya waandishi wa habari wakimfuatilia kwa makini Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mh. John Haule (hayupo pichani) wakati akielezea mafanikio mbalimbali ambayo Serikali ya Tanzania na Jamhuri ya Watu wa China zinajivunia kuyapata katika miaka 50 ya mahusiano ya kidiplomasia.
Habari/Picha zote na Eliphace Marwa- MAELEZO, Dar es Salaam.
Serikali ya Tanzania na Jamhuri ya Watu wa China zinajivunia kuadhimisha miaka 50 ya mahusiano ya kidiplomasia ambayo yamekuwa na mafanikio makubwa kwa nchi zote mbili tangu kuanzishwa kwake mwaka 1964.
Hayo yamesemwa jana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa kimataifa Mh. John Haule wakati akiongea na na waandishi wa habari katika ukumbi wa mikutano uliopo Idara ya Habari jijini Dar es Salaam.
Mh. Haule alisema moja ya vielelezo vikubwa vya ushirikiano wa nchi hizo mbili ni Reli ya TAZARA, Kiwanda cha Nguo cha Urafiki na kwa wapenzi wa Soka, ni Uwanja wa Kisasa wa Michezo wenye Uwezo wa kuchukua watu elfu sitini wakiwa wamekaa.
Aidha aliongeza kuwa Tanzania ilipata bahati ya kuwa nchi ya kwanza katika bara la Afrika kutembelewa na Mhe. Xi Jinping, Rais wa Jamhuri ya Watu wa China tangu ateuliwe kuwa Rais wa nchi hiyo ambacho ni kiashiria cha mahusiano mazuri baina ya nchi hizo mbili.
″Tangu kufanyika kwa ziara ya Mhe. Rais Xi Jinping nchini, takwimu ya idadi ya wageni wenye uraia kutoka China waliotembelea Tanzania kwasababu mbalimbali zikiwemo utalii na biashara imeongezeka kutoka 10790 kwa mwaka 2013 hadi kufikia 11555 kwa mwaka 2014. Pia idadi ya Watanzania waliotembelea nchini China imeongezeka kutoka 7657 kwa mwaka 2013 hadi kufikia 8114 mwaka 2014.″ alisema Haule.
Kwa upande wake Balozi wa China nchini Mh. Dkt. Lu Youqing alisema Serikali yake imekubali kuendelea kutoa mikopo nafuu kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali iliyopo katika mpango wa “Matokeo Makubwa Sasa- (BRN)” ambayo Serikali ya Tanzania tayari imekwisha iwasilisha kwa Serikali ya nchi yake.
″Vyombo vya Usalama vya Tanzania na China vimekubaliana kushirikiana ili kuimarisha usalama wa nchi hizi mbili hususani katika kupambana na uhalifu wa kimataifa kama vile biashara za pembe za ndovu, meno ya tembo na madawa ya kulevya″, alisema Balozi Lu.
Wakati wa ziara ya kihistoria ya Rais Xi Jinping iliyofanyika mwanzoni mwa mwaka 2013 jumla ya Makubaliano na Mikataba kumi na sita kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Watu wa China ilitiwa saini pamoja na misaada mbalimbali ya kibinadamu kutolewa.