Afisa habari kitengo cha habari Umoja wa mataifa nchini Tanzania(UNIC) Bi. Usia Nkhoma Ledama akizungumza katika viwanja vya Mazingira Senta mjini Shinyanga kwenye warsha ya siku moja iliyokutanisha shule 10 za sekondari, vyuo na walimu kutoka katika shule na vyuo hivyo vilivyopo katika manispaa ya Shinyanga, ambapo alisema Umoja wa Mataifa(UN) unalipa suala la elimu kipaumbele sana kwa wanafunzi hivyo kuwataka wanafunzi kuwa na malengo katika maisha yao kwa kusoma kwa bidii,kuepuka vishawishi vinavyopelekea kupata ujauzito wakiwa wanafunzi tena chini ya umri wa miaka 18.
Afisa habari huyo pia aLItumia fursa hiyo kuwatahadharisha wanafunzi wa kike kuepuka ngono kwani kwa mujibu wa utafiti wao takwimu zinaonesha kuwa vijana wa kike wenye umri wa miaka 15-19 wana uhusiano wa kingono na wanaume wanaowazidi miaka juu zaidi ya umri wao hivyo kuwepo kwa hatari ya kuambukizwa VVU na Mimba za utotoni.Kushoto ni Mwenyekiti wa taasisi ya Umoja wa Mataifa Tanzania (UNA) tawi la Shinyanga bwana Ezra Manjerenga.(Picha zote na Malunde1 blog ya Shinyanga)
Wanafunzi wa shule mbalimbali za sekondari Busurwa, Uhuru, Mazinge, Buluba, Chamaguha, Kizumbi, wakimsikiliza Afisa habari kitengo cha habari Umoja wa mataifa nchini Tanzania (UNIC) Bi Usia Nkhoma Ledama (hayupo pichani) ambaye alisema kwa mujibu wa sensa yao mwaka 2012 asilimia 65 ya Watanzania wote vijana wenye umri wa miaka chini ya 24,lakini pia asilimia 40 ya vijana wa kike wenye miaka chini ya 18 wanapata mimba za utotoni na wengine kuolewa katika umri huo.Aliongeza kuwa asilimia 23 ya vijana umri wa miaka 15-19 wameanza kuzaa na katika umri huo kati ya vijana wanne basi mmoja anaolewa ama kupata mimba.
Wanafunzi wa vyuo vya VETA, MUCCOBS, Shycom , waliohudhuria katika warsha hiyo ya Umoja wa Mataifa wakimskiliza Afisa habari kutoka UN, (hayupopichani) ambaye aliwataka kutumia fursa mbalimbali zinazotolewa na Umoja wa mataifa hapa nchini,lakini pia kuwaomba wazazi na walezi wa wanafunzi kujenga tabia ya kufuatilia mienendo ya watoto wao na kuwasaidia ili kuwafanya wapende elimu ili kufikia malengo ya Millenia.
Mjumbe wa asasi ya vijana ya Umoja wa Mataifa Tanzania, Bw. Innocent akizungumzia kuhusu klabu za Umoja wa Mataifa katika shule za sekondari na vyuoni ambapo alisema miongoni mwa faida ukiwa mwanachama wa klabu hizo ni kupata taarifa nyingi tena kwa wakati kutoka UN kuwa karibu na umoja wa mataifa, kuhudhuria mikutano ya UN, kupata nafasi ya kusaidia jamii lakini pia kuwajengea uwezo wa aina mbalimbali kama vile kuongea mbele za watu,kuandaa ripoti,kupata vyeti n.k
Walimu na wanafunzi waliohudhuria warsha hiyo wakifuatilia kilichokuwa kinajiri katika eneo la viwanja vya Mazingira Senta mjini Shinyanga ambapo maafisa kutoka Umoja wa Mataifa walieleza kazi za Umoja wa Mataifa na wakatumia muda fursa hiyo kuitaka jamii kubadilika na kuhamasisha jamii kufuata uzazi wa mpango ikiwa ni pamoja na kuwa tayari kupiga vita suala la vifo vya akina mama wajawazito na watoto,mimba za utotoni ambapo watoto wa kike milioni 7.5 miaka chini ya 18 wanazaa kila mwaka.
Mwenyekiti wa taasisi ya Umoja wa Mataifa Tanzania (UNA) tawi la Shinyanga, Bw. Ezra Manjerenga akimkaribisha mkuu wa wilaya ya Shinyanga ndugu Annarose Nyamubi katika warsha hiyo iliyokutanisha shule 10 za sekondari na vyuo vitatu vilivyopo katika manispaa ya Shinyanga. Katikati ni Mkutubi kutoka kitengo cha habari Umoja wa Mataifa nchini Tanzania(UNIC) Bi. Harriet Macha na wa kwanza kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Bi. Anna rose Nyamubi.
Mgeni rasmi katika warsha hiyo, Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Bi. Anna rose Nyamubi, ambaye ni mdau wa maendeleo na mwanafamilia wa Umoja wa Mataifa (siku za nyuma aliwahi kufanya kazi na Umoja wa Mataifa katika shirika la UNICEF), alisema nchi ya Tanzania inatekeleza malengo ya millenia kupitia ilani ya CCM katika kuwaletea maendeleo wananchi wake hususani katika kupunguza umaskini.
Katika hatua nyingine Bi. Nyamubi aliwataka vijana kuchangamkia fursa zinazotolewa na Umoja wa mataifa. Mkuu huyo wa wilaya aliongeza kuwa serikali inawajali vijana hivyo kuwataka kusoma kwa malengo kwani bila elimu dunia itawaacha na kuwataka kuacha kutegemea wazazi wao kwamba watarithi mali.
Aidha Nyamubi alitumia fursa hiyo kuwataka wazazi ambao hawajapeleka watoto wao kidato cha kwanza wawapeke haraka kabla ya kuwachukulia hatua.