Kila mwaka tarehe 23 Machi nchi wanachama wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani hujiunga na kuadhimisha kuzaliwa kwa Shirika hilo lililoanzishwa tarehe 23 Machi, 1950 kulingana na kauli mbiu. Kauli mbiu ya mwaka huu ni ’Ushirikishwaji wa Vijana katika Masuala ya Hali ya Hewa’- ”(Weather and Climate: Engaging Youth)”.
Katika kuadhimisha Siku ya Hali ya Hewa Duniani (WMO), Shirika la Hali ya Hewa linawahamasisha vijana ulimwenguni kote kujihusisha na masuala ya hali ya hewa, ili kupata maarifa na uelewa wa hatua za kuchukua katika kipindi hiki cha mabadiliko ya hali ya hewa duniani. Hatua hii ya WMO ni muhimu kwa ustawi wa kizazi hiki na kijacho ili kujenga jamii imara hapo baadae.
Siku ya Hali ya Hewa Duniani ni siku ya kutafakari Juhudi zinazofanywa na Wanasayansi Duniani katika kufahamisha Dunia kuchukua tahadhari juu ya mabadiliko ya hali ya hewa duniani na athari zake. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania inatoa wito kwa vijana wote kubadilika na kuchukua hatua za kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa katika kizazi hiki na kuchukua tahadhari ili kizazi kinachokuja waweze kufaidi dunia yenye mazingira bora zaidi.
Vijana wote walioko mashuleni vyuoni na wajasiriamali washiriki katika kuokoa dunia kutoka kwenye majanga yaletwayo na mabadiliko ya hali ya hewa. Aidha chachu kubwa ni kuhakikisha vijana wanakuwa mstari wa mbele katika kufuatilia taarifa za hali ya hewa zitolewazo na Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini.
Kama ilivyo kwa wanachama wengine, Tanzania inaungana nao kuadhimisha siku hii inayofikia kilele tarehe 23 Machi, 2014 kwa kuwakaribisha wananchi wote kutembelea vituo vya hali ya hewa nchini ili kuona shughuli zitolewazo na Mamlaka kuanzia tarehe 21-23 Machi 2014.
Aidha, Mamlaka itambelea na kutoa elimu kwa vijana wa baadhi ya shule na vyuo mbali mbali kupitia ofisi zake zilizopo nchini kuanzia tarehe 19-20 Machi 2014. Kutoa statements/makala za siku hiyo kwenye magazeti, vipindi kwenye radio, na televisheni kuhusu ushirikishwaji wa vijana katika masuala ya hali ya hewa.
Mamlaka inawatakia maadhimisho mema ya Siku ya Hali ya Hewa Duniani
’Ushirikishwaji wa Vijana katika Masuala ya Hali ya Hewa’
(Weather and Climate: Engaging Youth)