Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, leo, Alhamisi, Machi 20, 2014, amewasili mjini Dodoma kwa ziara ya kikazi ya siku tatu ambako miongoni mwa mambo mengine atakuwa Mgeni Rasmi na atahutubia Bunge Maalum la Katiba kesho, Ijumaa, Machi 21, 2014.
Muda mfupi baada ya kuwa amewasili na kulakiwa na Waziri Mkuu, Mheshimiwa Mizengo Peter Pinda kwenye Uwanja wa Ndege wa Mjini Dodoma, Rais Kikwete ameendesha Kikao cha Baraza la Mawaziri lake kwenye Ukumbi wa TAMISEMI ikiwa ni shughuli yake ya kwanza katika ziara hiyo fupi ya Mkoa wa Dodoma.
Kesho, Ijumaa, Rais Kikwete atakuwa mgeni rasmi na atahutubia Bunge Maalum la Katiba kutokana na mwaliko wa Mwenyekiti wa Bunge hilo, Mheshimiwa Samuel J. Sitta ambaye alimwalika Rais Kikwete kwa barua yake ya Machi 15, mwaka huu, ambayo ilijibiwa Machi 18, mwaka huu, kwa Rais Kikwete kukubali mwaliko huo.
Mwaliko huo wa Mheshimiwa Sitta kwa Rais Kikwete umetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 7(1) (g) na Kanuni 75 (1) ya Kanuni za Bunge Maalum ambazo zinampa Mwenyekiti wa Bunge Maalum madaraka ya kumwalika Mgeni Rasmi aweze kuhutubia Bunge Maalum.