Sehemu ya kwanza
UKUTA NI MATOKEO YA UCHAGUZI ULIOPITA.
Na Peter Sarungi (Next Speaker).
Uchaguzi uliopita 2015 ulikuwa ni uchaguzi wa kihistori toka siasa ya vyama vingi ulipoanza nchini. Ulikuwa ni uchaguzi ambao tulishuhudia maajabu mengi ambayo hatukuwahi kuyaona katika chaguzi zilipita. Tuliona miiko ya vyama ikivunjwa, vigogo maarufu wakihama kambi zao za miaka mingi na wengine kustaaf gafla siasa kwa shinikizo mbalimbali, tuliona mbwembwe nyingi na maigizo mengi ya jukwaani, tuliona kejeli na kashfa nyingi, tuliona misukosuko mingi ya polisi dhidi ya wanasiasa, tuliona matamko mengi ya makundi mbalimbali ya jamii juu ya wagombea, tulishuhudia usaliti mkubwa, tuliona kampeni zilizo andaliwa kwa kiwango cha juu na za garama za juu kabisa kuwahi kutokea Tanzania, tulishuhudia kambi zikifanya kazi isiyokuwa na malipo usiku na mchana bila kulala, tulishuhudia mafuriko ya kila aina kwa kambi zote, tulishuhudia mbinu chafu na safi zilizotumika, tulishuhudia uvumilivu na ustaimilivu mkubwa kwa wananchi wa kambi zote, tulishuhudia vifo vya gafla na vya mshituko kwa baadhi ya wanasiasa wakubwa (R.i.p all), tulishuhudia kesi tata na kuntu za kutafsiri katiba, tulishuhudia upindishwaji wa baadhi ya vifungu na makatazo, tulishuhudia mihemko na hari kubwa ya vijana na wanawake kwenye siasa, tulishuhudia matumizi makubwa ya teknohama na mitandao ya kijamii, tulishuhufia idadi kubwa ya wananchi waliojitokeza kupiga kura lakini vilevile tulishuhudia matokeo ya kura tulizopiga (CDM 6M, CCM 8M).
Bila kupepesa macho na mdomo, uchaguzi huu 2015 ulikuwa wa mnyukano mkali sana uliotikisa nchi kwa kila nyanja ya uchumi, siasa, jamii na kimataifa. Ni uchaguzi ulifuatiliwa na mataifa mengi ya nje na majirani zetu, wengi walitaka kuona ukomavu wa kidemokrasia kwa nchi yetu hasa kigogo mmoja alipoamua kupambana na kambi aliyo lelewa tangu aanze siasa. Kambi zote zilikuwa na imani na mategemeo makubwa ya kushinda uchaguzi. Tume na mabadiliko yake ya mara kwa mara nayo ilijinasibu kwa watanzania kuwa itatenda HAKI.
Kwa hayo yote yaliyofanyika kipindi cha uchaguzi ni dhairi na ukweli usiopingika kuwa Uchaguzi huu umeacha VIDONDA ambavyo mpaka sasa bado ni vibichi kabisa vinavyohitaji kutibiwa haraka ili walau vibadilike na kuwa makovu yanayotoweka taratibu. Na vidonda hivi ndivyo vinavyozalisha operation kama hii ya UKUTA. Maranyingi tunapoenda msibani utakuta watu wengi wanalia kwa uchungu wa misiba ya wapendwa wao waliotangulia kabla ya msiba huo, yaani unakuta mtu anaenda kwenye msiba wa jirani yake lakini analia kwa uchungu huku akikumbuka mpendwa wake aliyefariki miaka ya nyuma. Vivyo hivyo katika operation hii ya UKUTA wengi watashiriki kuandamana kwa maumivu waliyoyapata katika uchaguzi uliopita. Hii ni kawaida kabisa ya binadamu kupata sehemu ya kutoa hisia zake na kuelezea maumivu yake ili awe huru na maisha yaendelee.
Ningekuwa mimi ni Raisi wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania, kama alivyo JPM, Ningeanza na kutibu vidonda vilivyosababishwa na uchaguzi maana ni wengi walio umia na matokeo ya kushindwa. Unapokuwa Raisi wa nchi maana yake unakuwa Raisi wa raia wote bila kujali itikadi zao na bila kujali kama walikuchagua ama laa. Na kwa sababu hii ni siasa basi ukiwa kama raisi unapata nafasi nzuri ya kuwarudisha na kuongeza imani kwa wale ambao hawakukuchugua.
Mimi Ningeunda baraza ama kamati ya kutibu haya maumivu yaani chombo cha usuluhishi na kujenga umoja wa kitaifa. Chombo hichi kingekuwa na kazi kuu mbili, 1. Kurejesha umoja wa kitaifa kuanzia juu kwa viongozi hadi chini kwa wananchi, 2. Kushugulika na mapungufu yaliyojitokeza wakati wa uchaguzi kwa kila idara. Naamini hii ingesaidia sana utawala wa JPM maana sio afya hata kidogo kudharau na kubeza kura 6M za upande wa pili kwa mamlaka uliyopata kwa kura 8M. Hizi kura 6M ni watu wa makundi mbalimbali ya jamii na wa rika tofauti na ni watanzania wenye haki katika nchi yao, kuwaweka kando na kubeza uwepo wao ni kosa kubwa kisiasa kiuchumi na kwa ustawi wa jamii.
#MyTake Mhe. John Pombe Magufuli nakushauri uunde chombo hicho cha usuluhishi na kujenga umoja wa kitaifa ili kuondokana na vikwazo kama hivi katika utawala wako maana yawezekana haya yakajitokeza kwa wingi mbeleni. Unaweza kukiunda kabla ya UKUTA ama baada ya UKUTA.
Tupo wengi tunaopenda aina ya uongozi wako maana madhaifu ni machache kuliko mazuri na tungependa kuendelea kula matunda ya uongozi wako kwa kipindi chote bila kikwazo.
Asanteni sana.