Mwandishi Wetu, Moshi
KATIKA kuelekea mchezo wa jana dhidi ya Flamingo FC ya Arusha, Machava FC ambo ndio mabingwa wa ligi daraja la Tatu, mkoa wa Kilimanjaro, wamekabidhiwa vifaa vya michezo na uongozi wa chama cha Mapinduzi CCM wilaya ya Moshi.
Machava FC walikabidhiwa vifaa hivyo ambavyo ni mipira mitano na Jezi, kama sehemu ya mchango wa Chama hicho kwa timu hiyo ambayo kwa sasa ndio inayobeba Roho ya mkoa wa Kilimanjaro katika medani ya soka.
Akizungumza baada ya kukabidhi vifa hivyo vilivyotolewa kwa timu hiyo na Mjumbe wa Halmashauri kuu CCM, Jerry Slaa, Katibu wa CCM wilaya ya Moshi Mjini Aluu Segamba aliwahakikishia wapenzi wa soka mkoani hapa kuwa wako tayari kushirikiana nao hadi mwisho wa Safari.
“Leo tunatimiza ahadi yetu kwa wawakilishi wetu, mabingwa wa Mkoa timu ya Machava, tunaamini kuwa timu hii kama roho ya kilimanjaro katika mchezo wa soka itafanya makubwa na kinachotakiwa ni kuwapa sapoti inayostahili,” alisema Segamba.
Naye Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo Abuu Masoud, baada ya kupokea msaada huo kutoka CCM, alisema kutokana ushirikiano unaoneshwa na wadau wa soka kwa timu yao wanaahidi kufanya vizuri katika michezo yao yote na kuwapa raha wapenzi na mashabiki wa Machava mkoani Kilimanjaro.
Kwa upande kocha msaidizi wa machava aliwaondoa hofu mashabiki wa timu yake kuhusu hali ya Afya ya mshambuliaji wa kutumainiwa wa klabu hiyo, Isa Kipese na kuelekea mchezo wa jana na kuongeza kuwa kinachosubiriwa ni ripoti za madaktari wanaomshughulikia mchezaji huyo.
Machava FC ambayo inauwakilisha mkoa katika michezo ya Mabingwa wa mikoa imekuwa ikipokea sapoti kutoka kwa wadau wa michezo mkoani hapa ambapo hivi karibuni tu Mbunge wa Moshi Mjini, Filemon Ndesamburo na Mstahiki Meya wa Moshi, Jafary Michael walitembelea kambi ya timu hiyo na kuchangia fedha taslimu shilingi laki saba.
Akikabidhi vifaa hivyo, mipira miwili na Jezi kwa diwani wa kata ya Kaloleni, Michael Mwita, Segamba alisema kuwa wanalenga kuunganisha umma wa mkoa wa Kilimanjaro, kupitia michezo na kuongeza kuwa katika swala la michezo watu wote ni ndugu bila kujali itikadi zao.