Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) limedhamini tamasha la watoto lijulikanalo kwa jina la 'Toto Party' linalotarajiwa kufanyika Desemba 25 na 26 mwaka huu katika ufukwe wa Cine Club jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Kampuni ya Glitz Entertainment Limited, ambao ni waandaaji wa tamasha la TOTO PARTY, Bw. Dennis Ssebo alisema kuwa anawashukuru NSSF kwa kuwaunga mkono na kuongeza udhamini wao kwa tamasha hilo la Toto Party'
“Nawashukuru sana Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) kwa kuungana na sisi katika kutoa burudani ambayo itawafikia watu wengi zaidi katika sherehe za Noeli na Boxing Day”, Alisema Bw. Ssebo.
Katika sherehe hizo mbili NSSF watatoa zawadi za vitabu pamoja na karamu kwa kila mtoto atakayehudhuria vile vile watapata kucheza michezo mbalimbali kama soka la ufukweni, kuogelea, kusaka hazina (Treasure hunt) na kujipaka rangi usoni (Face painting) na mengine mengi.
Mbali na watoto kucheza na kufurahi michezo mbalimbali pia wazazi wao watachuana katika mchezo wa kuvuta kamba ambapo washindi katika michezo hiyo watazawadiwa zawadi mbalimbali na viingilio ni Sh 3,000 kwa watoto na wakubwa Sh 7,000.
Waratibu wa sherehe pia wamebainisha kuwa mwakani mbali na Dar es Salaam, sherehe hizo pia zitafanyika kwenye katika mikoa ya Arusha na Tanga.