Tafiti zinaonyesha kuwa nyama nyekundu ikitumiwa kwa wingi ni kati ya vyakula vinavyosababisha aina mbali mbali za saratani kama ile ya kinywa, koo, utumbo mpana, mapafu na kongosho.
Vile vile, nyama nyekundu ina lehemu kwa wingi ambayo huweza kuongeza hatari ya kupata magonjwa ya moyo, shinikizo kubwa la damu, saratani, kisukari na kiharusi.
Kama unatumia nyama nyekundu unashauriwa isizidi nusu kilo kwa wiki. Inashauriwa zaidi kutumia nyama nyeupe, ambayo ni pamoja na kuku, bata, bata mzinga na samaki. Nyama nyekundu ni kama nyama ya ng’ombe, mbuzi, kondoo, nguruwe na sungura.
Je, nyama zilizosindikwa zina madhara gani?
Nyama zilizosindikwa zimethibitishwa kuongeza hatari ya kupata saratani hata zikitumiwa kwa kiasi kidogo tu. Nyama hizi zinahusishwa na saratani za kinywa, koo, tezi la kiume(prostate), utumbo mpana na mapafu.
Inashauriwa kuepuka nyama zilizosindikwa. Nyama hizo ni pamoja na zile zilizosindikwa au kuhifadhiwa kwa chumvi, mafuta, kemikali au kukaushwa kwa moshi. Mfano wa nyama hizo ni soseji, nyama za kopo, hot-dog, salami na bacon