Quantcast
Channel: HABARI NA MATUKIO
Viewing all articles
Browse latest Browse all 19575

MATANGAZO YA DIJITALI KUANZA KESHO JIJINI DAR ES SALAAM

$
0
0
SERIKALI kwa kupitia Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, imetangaza rasmi kuwa kuanzia kesho Desemba 31, Tanzania itaanza kuingia kwenye mfumo mpya wa urushaji wa matangazo wa kutoka Analogy kwenda kwenye Digitali.

Taarifa ya Naibu Waziri, January Makamba, ilisema kuwa uamuzi huo unatokana na kurejea tangazo lao la Februari 23 mwaka huu juu ya usitishwaji wa matangazo ya televisheni kwa kutumia teknolojia ya analojia kwenda teknolojia ya dijitali.

Makamba alisema maandalizi ya kuzima mitambo ya analojia kuanzia 31 Desemba 2012 yamekamilika kwa mujibu wa makubaliano ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Hata hivyo, serikali ilitangaza kuwa uzimaji wa mitambo ya analojia utafanyika kwa awamu kama ifuatavyo, ikianzia na jiji la Dar Es Salaam-31 Desemba, Dodoma & Tanga, Januari 31, Mwanza Februari 28, Moshi & Arusha Machi 31, wakati Mbeya itakuwa ni Aprili 30.
“Tumeamua kuanza kuzima mitambo hiyo kwa Jiji la Dar es Salaam kwanza ili kutoa fursa kwa makampuni yenye leseni kusimika mitambo ya utangazaji wa dijitali katika mikoa mingine, huku tukiamini kuwa makampuni hayo yamejipanga kukamilisha usimikaji wa mitambo hiyo katika mikoa minane katika miezi minane ijayo.

”Mitambo ya analojia itakayozimwa kesho ni ile iliyopo Kisarawe na Makongo. Vituo ambavyo siku ya tarehe 1 Januari 2013, vitapaswa kuanza kutangaza matangazo kwa mfumo wa dijitali ni TBC1, ITV, EATV, Channel 10, StarTV, DTV, CapitalTV, TumainiTV, ATN, MlimaniTV, C2C, CTN, CloudsTV na Efatha,” alisema.

Alisema Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inafanya jitihada za kutosha kuhakikisha kwamba makampuni yenye leseni za kusambaza ving’amuzi yanakuwa na ving’amuzi vya kutosha na vingine vimeagizwa ili kukidhi mahitaji ya baadaye na vile vilivyopo sokoni vina ubora unaokubalika.

Vilevile, Serikali kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania itahakikisha kwamba zoezi la uhamaji linafanyika bila usumbufu na kero kwa wananchi. Makampuni yanayouza ving’amuzi yameagizwa yaimarishe huduma kwa wateja wakati wa kuuza ving’amuzi na hata baada ya ununuzi iwapo wananchi watakuwa na matatizo na ving’amuzi.

”Zoezi hili la uhamaji ni muhimu sana kwa maendeleo ya nchi yetu. Tutakapokuwa tumekamilisha uhamaji, huduma za mawasiliano na utangazaji zitapanuka na kuwa bora zaidi. Kwa mfano, itawezekana sasa kuangalia televisheni kupitia simu zetu za mikononi.
“Vilevile, itawezekana, kwa bei nafuu kabisa, kwa mtu mwenye uwezo wa kutengeneza vipindi kukodisha chaneli yake na kutangaza vipindi vyake. Vilevile, bei za mawasiliano na utangazaji zitashuka, na tutakuwa tumepiga hatua kubwa kwenye mapinduzi ya teknolojia duniani, ambayo nchi yetu haiwezi kubaki nyuma,” alisema.

Makamba alisema serikali kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania itaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu uhamaji huu na kutarajia kupata ushirikiano wa karibu kutoka kwa wadau wa sekta ya utangazaji na wananchi kwa ujumla katika kipindi cha uzimaji wa mitambo ya utangazaji wa televisheni ili kufanikisha zoezi la uzimaji wa mitambo ya utangazaji ya teknolojia ya analojia.

Uhamaji huu hautahusu televisheni za wananchi zinazopata matangazo kupitia madishi (nyungo) (satellite) au nyaya (cables). Hivyo, wananchi wanaopata matangazo kupitia DStv, Zuku, na nyinginezo wataendelea kupata matangazo yao kama kawaida.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 19575

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>