WATU sita wameripotiwa kupoteza maisha kutokana na wivu wa mapenzi, katika matukio matano tofauti katika kipindi cha miezi mitatu mkoani Mbeya.
Matukio hayo yametokea kati ya Oktoba, Novemba mwaka jana na Februari mwaka huu, ambapo jeshi la Polisi limefanikiwa kuwatia mbaroni watuhumiwa wa mauaji hayo ya mapenzi.
Akizungumza na mtandao huu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Diwani Athumani, (pichani) alisema kuwa katika mauaji hayo watuhumiwa watano wamefikishwa mahakamani kwa hatua zaidi ya kisheria.
Alisema tukio la kwanza, lilitokea Februari 15, mwaka huu katika Kijiji cha Kambi Katoto wilayani Chunya, ambapo marehemu Sadock Richard, ambaye ni mkazi wa kijiji hicho aliuawa kwa wivu wa mapenzi.
“Kutokana na tukio hilo watuhumiwa wawili tulifanikiwa kuwatia mbaroni, ambao ni John Maiko na Kulwa Maiko wote hawa ni ndugu wa familia moja. Walimchangia marehemu kwa kumpiga na kumkata panga kwenye paji la uso na kusababisha kifo chake.
“Chanzo cha mauaji hayo ni wivu wa mapenzi, ambapo watuhumiwa wakiwa kwenye ukumbi wa starehe, walikuwa wakicheza disko mtuhumiwa John Maiko alimuona mpenzi wake Sarafina Joseph akicheza na marehemu Sadock, ambaye naye alikuwa na mahusiano na binti huyo.
“Ugomvi huo inadaiwa marehemu aliwazidi nguvu watuhumiwa ambao waliamua kutoka nje na kwenda kuchukua panga kisha kumkata Sadock kwenye paji la uso. Na katika tukio la pili ni kuuawa kwa Daniel Mwasalemba (18), mkazi wa Itiji ambaye alichomwa na kitu chenye ncha kali, kutokana na wivu wa mapenzi,” alisema Kamanda Diwani.
Alisema kutokana na mauaji hayo, jeshi la Polisi lilifanikiwa kumkamata Peter Bosco (25) kwa kuhusika na mauaji hayo kwani marehemu na mtuhumiwa walikuwa wakimgombania mwanamke Elizabeth Michael (18), ambaye naye ni mkazi wa kijiji hicho.
Kamanda huyo wa Polisi wa mkoa, alisema kuwa katika tukio la tatu ni kuuawa kwa mwanamke Taines Kombani (32) mkazi wa Kata ya Isuto wa Mbeya vijijini, ambaye ameuawa kwa kupigwa ngumi na mateke na mumewe.
Kutokana na tukio hilo jeshi la polisi bado linaendelea na msako wa kumtafuta mtuhumiwa wa mauaji hayo, ambaye inadaiwa alitoa onyo kwa mke wake kutotembea na wanaume wengine.
Katika tukio la nne polisi inamshikilia Hamad Jackson (40) mkazi wa Kijiji cha Igodima wilayani Chunya kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya mkewe Vumilia Halifa (30) mkazi wa Igodima, ambaye alimpiga kwa sururu kichwani.
“Katika tukio la tano, jeshi letu linamshikilia Willson Whatson Mkazi wa Kijiji cha Ivugula Wilayani Mbozi, kwa tuhuma za mauaji ya watu wawili kwa kile kinachosemekana ni wivu wa mapenzi.
“Mauaji haya yamefanyika katika Kijiji cha Ivugula, ambapo mtuhumiwa Whatsoni anadaiwa kuhusika na mauaji ya Andson Mwashambwa (51), ambaye ni mganga wa kienyeji na bwana shamba Mgala (41) wote wakazi wa Mlowo-Rutumbi,” alisema.
Kamanda, alisema chanjo cha mauaji hayo ni wivu wa mapenzi, ambapo marehemu Andson Mwashambwa akiwa na rafiki yake walimkuta Willsoni akiwa na mkewe aitwaye Anna Kaswisa na kuanza kuwashambulia.