WASANII mahiri nchini Naseeb Abdul 'Diamond Platnumz' na Mzee Yusuf wamewaahidi mashabiki wa burudani hususani wa Jiji la Dar es Salaam kutokosa kesho katika Ukumbi wa Dar Live kushuhudia shoo ya kibabe inayotambulika kama Tamasha la Wafalme.
Wakiongea na wanahabari katika Ofisi za Kampuni ya Global Publishers Ltd zilizopo Mwenge-Bamaga jijini Dar, wakali hao wamesema wamejiandaa vilivyo kwa ajili ya shoo hiyo itakayoacha historia katika pande za Mbagala-Zakhem, jijini Dar.
Naye Meneja wa Dar Live, Abdallah Mrisho amewataka mashabiki wa burudani kuhudhuria kwa wingi kesho katika Uwanja wa Taifa wa Burudani, Dar Live maana kila kitu kiko safi kuanzia ulinzi na huduma zote muhimu.
Shoo hiyo ya aina yake itaanza asubuhi kwa burudani za watoto ambapo kundi la sarakasi la Masai Worriors litahakikisha linatoa burudani ya nguvu kwa watoto wote kwa kuwapa staili mbalimbali za sarakasi na mazingaombwe.
Pia watoto wataburudika na michezo kibao kama vile kuogelea, kubembea, kuteleza huku kila mmoja atakayehudhuria kurudi na zawadi kemkem nyumbani kwao.
Kiingilio cha Tamasha la Wafalme kitakuwa shilingi 10,000 kawaida wakati kwa VIP kiingilio kikiwa shilingi 20,000.
WOTE MNAKARIBISHWA!