Katibu Mkuu wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo (Taswa), Amir Mhando akifafanua jambo kuhusu maandalizi ya hafla ya utoaji wa tuzo kwa wanamichezo bora wa mwaka ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein. Kushoto ni Mjumbe wa Tawsa, Mwani Nyangasa na Makamu Mwenyekiti wa Taswa, Egbert Mkoko. (Picha na Francis Dande)
Na Mwandishi Wetu
RAIS wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Dk. Ali Mohamed Shein, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika sherehe ya Tuzo za Wanamichezo Bora wa Mwaka, zinazoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA).
Tuzo hizo zinatarajiwa kufanyika kesho, katika Ukumbi wa Diamond Jubilee, ambapo jumla ya tuzo 46 zinatarajiwa kutolewa kwa wanamichezo mbalimbali, sambamba na Tuzo ya Heshima ambayo ilitwaliwa kipindi kilichopita na Rais Mstaafu, Benjamin William Mkapa.
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam, Makamu Mwenyekiti wa Taswa, Egbert Mkoko alisema, tuzo hizo zinatarajiwa kuwa za aina yake, ambazo zitatolewa sanjari na pesa taslim kwa washindi.
Mkoko alisema, wanazingatia mambo mbalimbali ili mtu aweze kuwa mshindi katika tuzo hizo, ambayo ni mchango wa mchezaji husika katika timu yake pamoja na timu ya Taifa, nidhamu ya mchezaji ndani na nje ya uwanja, uhusiano wake na jamii inayomzunguka, kipaji cha kipekee kwa mchezaji husika.
Vigezo vingine walivyoangalia ni awe mwamasishaji na mwenye ushawishi kwa wenzake, huku kigezo cha ziada, mchezaji asiwe anatumia dawa zinazozuiliwa michezoni.
Aidha Mkoko alisema, kwa upande wa burudani ambayo itaburudisha siku hiyo, bado wanaendelea na mazungumzo na bendi mbalimbali.