Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.
Tigo Tanzania imeshinda tuzo ya “Huduma Bora ya Kibunifu” kutokana na huduma yake ya kutuma na kupokea fedha kimataifa kati ya Tigo Pesa Tanzania na Tigo Cash Rwanda katika kongamano na maonyesho ya kimawasiliano barani Afrika ijulikanayo kama AfricaCom iliyofanyika Cape Town, Afrika Kusini hivi karibuni.
Meneja Mkuu wa Tigo Tanzania, Diego Gutierrez, alisema kwamba tuzo hii ni matokeo ya kuwa na mwaka wenye mafanikio tele katika huduma zake za kifedha, Tigo Pesa, ambayo imeweza kupiga hatua kubwa na kusababisha huduma hiyo kupaa kitaifa na kimataifa.
“Ni heshima kubwa kuweza kufika kwenye sita bora na hatimaye kuweza kunyakua ushindi wa tuzo ya AfricaCom 2014 katika Huduma Bora ya Kibunifu. Huu ni udhihirisho tosha wa ubunifu wetu kwa ajili ya kutoa huduma zilizo bora zaidi kwa wateja wetu wanaotumia huduma yetu ya kutuma na kupokea fedha kupitia simu,” alisema Gutierrez wakati akizungumza na waandishi wa habari kutoka makao makuu jijini Dar es Salaam.
Aliongeza, “Huu umekuwa mwaka mzuri sana kwetu katika huduma za kifedha kupitia simu. Tumeweza kuwa wa kwanza kuanzisha na kuzindua huduma ya kwanza ya kutuma na kupokea fedha ya kimataifa yenye uwezo wa kubadilisha moja kwa moja ankara ya fedha kati ya Tigo Pesa na Tigo Cash Rwanda ambayo imeweza kushinda tuzo hiyo ya AfricaCom 2014.
Huduma ingine ya kwanza duniani ambayo tumeweza kuianzisha na kuzindua mwaka huu ni gawio la Tigo Pesa kwa wateja wetu ambao wameanza kupokea marejesho ya fedha kila baada ya miezi mine katika akaunti zao za Tigo Pesa, ambayo imeweza kutusaidia kutimiza wajibu wetu wa kuwajumuisha wale ambao hawajafikiwa bado na huduma za kifedha kupitia simu.”
Huduma zingine za kibunifu ambazo Tigo imeweza kuzindua mwaka huu pia ni ushirikiano kati ya Tigo, Airtel na Zantel ambao inawaruhusu wateja kuweza kutuma na kupokea fedha moja kwa moja katika akaunti za mitandao hii ya simu bila ukiritimba wowote.
Mapema mwaka huu, kampuni iliweza kushirikiana na benki 17 nchini Tanzania ili kuwawezesha watumiaji wa Tigo Pesa, kutuma na kupokea fedha kwa akaunti zao za benki kutoka kwenye mifuko yao ya Tigo Pesa. Hii inawapatia wateja wetu fursa ya kupata huduma ya kutoa na kuweka fedha kupitia Tigo Pesa na akaunti zao za kibenki kwa masaa ishirini na nne.
“Napenda kuwashukuru wateja wetu wa Tigo Pesa milioni 3.6 ambao wamekuwa wakitumia huduma zetu kila siku. Wao ndio uti wa mgongo wa motisha yetu Tigo kuweza kufanya vizuri zaidi, pamoja na kuja na huduma za kibunifu zaidi,” alisema Gutierrez.
AfricaCom ni kongomano na maonesho ya kimawasiliano ya kila mwaka barani Afrika. Ilifanyika Cape Town, Afrika Kusini kati ya tarehe 11 – 13 Novemba, 2014.
Tuzo za mwaka huu ziliweza kujumuisha mashindano ya tuzo 16 tofauti katika sekta ya mawasiliano kuanzia kwenye masuala ya mtandao mpaka mambo ya masoko.