Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.
Baada ya makada mbalimbali wa CCM kutangaza nia ya kugombea urais kwenye Uchaguzi Mkuu ujao, Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa anasema bado hajaona mtu mwenye sifa ya kupewa nafasi hiyo kubwa nchini miongoni mwa waliojitokeza.
Hadi sasa ni makada wa CCM pekee waliotangaza nia hiyo ya kumrithi Rais Jakaya Kikwete, wakati vyama vya upinzani vimeingia makubaliano ya kumteua mgombea mmoja kupambana na chama hicho tawala.
Pamoja na wanasiasa wazito wa CCM kutangaza nia ya kugombea urais na baadhi kuanza harakati kabla ya kutangaza, Mchungaji Msigwa anasema wote waliojitokeza hawana dira ya kuipeleka nchi sehemu fulani kutoka hapa ilipo na hivyo hawastahili kupewa nafasi hiyo.
Akizungumza katika mahojiano mwishoni mwa wiki iliyopita kuhusu mambo mbalimbali ya kisiasa na kijamii, Msigwa alisema kujitangaza kwao siyo tatizo, lakini haoni kama kuna mtu mwenye sifa za urais. “Ukimuuliza kila mmoja kwa waliojitangaza kwamba ana vision (dira) gani kwa ajili ya nchi katika miaka mitano ijayo, wengi watatoa ahadi badala ya kueleza ataifikisha nchi wapi katika muda huo,” alisema mchungaji huyo bila ya kutaja majina ya waliojitokeza.
“Wengi kati ya hawa wanaojitangaza wanataka power (madaraka) ya kulinda status quo (nafasi zao), lakini nakuhakikishia hawana ‘vision’. Wanatumia hela zao kununua madaraka.”
Alisema hata siku moja mti wa mwembe haujawahi kumwita mtu akatungue maembe, bali msimu ukifika watu hufuata mti na kutungua maembe, akimaanisha wanaojitangaza sasa hawajafuatwa na mtu wajitangaze. “Tunahitaji mtu mwenye dira nzuri na si watu ambao watatupa ahadi ambazo hazitekelezeki,” aliongeza mchungaji huyo wa Iringa Vineyard Church na ambaye pia ni mratibu wa taifa wa kanisa hilo.
Pia, Mchungaji Msigwa alisema ni wapinzani pekee ambao wana mtu ambaye ana dira na ambaye wakati ukifika atajitokeza kutangaza kuwania kuingia Ikulu.
“Katika Ukawa viongozi wetu wakiafikiana na tukapata mtu mwenye maono ambaye ana anakubalika pia anaweza kupambana na mambo, tutafanikiwa,” alisema.
Akizungumzia makubaliano ya vyama vya upinzani kusimamisha mgombea atakayeungwa mkono na wote katika ngazi zote kuanzia Serikali za Mitaa alisema, “Kuna tofauti kati ya mwanasiasa na kiongozi. Mwanasiasa ni mtu anayependa kufanya mambo mazuri, lakini kiongozi ni mtu anayefanya mambo sahihi,” aliongeza:
“Mtu anayefanya jambo sahihi mara nyingi anafanya kwa kuwa jambo hilo linakuwa linaumiza, lakini mtu anayefanya mambo mazuri siku zote anafurahia.
“Siasa za siku hizi zimebadilika, hivyo mtu anayezifanya lazima ajue kwamba kuwa mwanasiasa na kuwa kiongozi ni vitu viwili tofauti.”
Hivyo alisema ni muhimu kwa wananchi kuwachunguza hao wanaojitangaza kuwania urais na kuzijua tabia zao kuanzia sasa. “Ukichagua mwizi, lazima atakwenda kuiba kwa sababu ndiyo tabia yake, hivyo ni lazima tuwachunguze, tuwajue ili tusije kuchagua watu wenye hulka ya wizi,” alisisitiza na kuongeza: “Tuwachunguze hawa watu na tusikurupuke.”