Shirika la Afya Duniani – WHO limesema kuwa idadi ya watu waliofariki dunia baada ya kuugua ugonjwa wa Ebola imeongezeka na kufikia zaidi ya Elfu Nne na Mia Nne (4,447), huku idadi kubwa ikiwa ni kutoka katika nchi za Afrika Magharibi.
Naibu Mkurugenzi Mkuu wa WHO - Bruce Aylward alisema ndani ya kipindi cha miezi miwili kuanzia hivi sasa idadi ya watu wanaougua Ebola huenda ikaongezeka na kufikia Elfu Kumi kama jitihada zaidi hazitafanyika za kukabiliana na ugonjwa huo.
Lakini hata hivyo Aylward alisema kuwa katika baadhi ya maeneo maambukizi ya ugonjwa huo wa Ebola yameanza kupungua.
WHO imezitaja nchi za Sierra Leone, Liberia na Guinea kuwa ndizo zilizoathiriwa zaidi na ugonjwa huo.
Mpaka sasa dunia inajikokota katika vita vyake dhidi ya Ebola huku maelfu ya watu wakiwa katika hatari ya kuambiukizwa ugonjwa huu ifikapo Disemba mwakani.