Quantcast
Channel: HABARI NA MATUKIO
Viewing all articles
Browse latest Browse all 19575

TAIFA STARS YATOLEWA MASHINDANO YA AFCON BAADA YA KUCHAPWA 2-1 NA MSUMBIJI

$
0
0




Shomary Kapombe akilia baada ya mechi.

Na Mahmoud Zubeiry, MAPUTO

MAREFA WA Uganda, wakiongozwa na Dennis Batte leo wameitupa nje ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika Tanzania, baada ya kuwapendelea waziwazi Msumbiji katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Zimpeto mjini hapa na kupata ushindi wa mabao 2-1.

Matokeo hayo yanamaanisha, Tanzania au Taifa Stars imetolewa katika hatua ya mwisho ya mchujo ya kuwania kupangwa kwenye makundi ya kuwania tiketi ya AFCON mwakani nchini Morocco kwa jumla ya mabao 4-3, baada ya awali kulazimishwa sare ya 2-2 Dar es Salaam.

Mambas inaingia moja kwa moja kwenye kundi lenye timu za Cape Verde, Niger na Zambia kupigania tiketi ya AFCON ya mwakani Morocco.

Kapombe akimtoka beki wa Msumbiji
Refa Dennis Batte akisindikizwa na Polisi na mbwa baada ya mechi
Mbwana Samatta akilia baada ya mechi
Hadi mapumziko, tayari Msumbiji walikuwa mbele kwa bao 1-0, lililofungwa na Josimar Machaisse dakika ya 45 aliyeunganisha krosi kutoka upande wa kulia.

Stars ilicheza kwa kujihami tangu mwanzo na kujibebesha mzigo wa kudhibiti mashambulizi mfululizo ya Mambas, huku yenyewe ikishambulia kwa kushitukiza.

Pamoja na mfumo huo, mashambulizi machache ya Stars yalikuwa yenye uhai na kama si refa Dennis Batte kuwabeba wenyeji, Tanzania ingemaliza na bao kama si mabao dakika 45 za kwanza.

Batte alikataa bao zuri la kichwa la beki Said Mourad aliyeunganisha mpira wa adhabu wa Khamis Mcha ‘Vialli’ baada ya Thomas Ulimwengu kuangushwa dakika ya 17.

Mshika kibendera nambari moja alimnyooshea kibendera cha kuotea mshambuliaji John Bocco akiwa anakwenda kufunga, wakati alikuwa hajaotea dakika ya 44.

Hali hiyo iliwakasirisha makocha wa Stars wakiongozwa na bosi wao, Mart Nooij waliokwenda kumkaripia mwamuzi huyo. Batte alisogea kwenye benchi la Tanzania na kuwaonya maofisa hao.

Kipindi cha pili, kocha Mholanzi alianza na mabadiliko Stars, akimuingiza kiungo Amri Kiemba kwenda kuchukua nafasi ya Khamis Mcha ‘Vialli’.

Mabadiliko hayo yaliibadilisha Stars pia na kuanza kutawala mchezo, wakifanya mashambulizi mfululizo langoni mwa Mambas. Hata hivyo, refa Batte na wasaidizi walitumia ujanja wa kitaaluma kupunguza kasi na mipango ya Stars kusaka mabao.

Kila wachezaji walipopamiana, mpira ulielekezwa kwa Tanzania- wachezaji wa Msumbiji walikuwa wana maisha mazuri mno mbele ya marefa wa Uganda leo.

Pamopja na yote, mshambuliaji wa TP Mazembe ya DRC, Mbwana Ally Samatta aliifungia Stars bao la kusawazisha dakika ya 75 baada ya kumkokota beki wa Mambas hadi karibu na lango la Msumbiji kabla ya kufumua shuti lililomshinda kipa Dario Khan.

Baada ya bao hilo, kasi ya mashambulizi ya Stars iliongezeka hasa baada ya kuingia Mrisho Ngassa aliyekwenda kuchukua nafasi ya Thomas Ulimwengu na Simon Msuva aliyechukua nafasi ya John Bocco.

Hata hivyo, refa Batte na wasaidizi wake waliendelea kuifanyia ‘roho mbaya’ Tanzania akiua mashambulizi na kuwaruhusu wachezaji wa Msumbiji kucheza na muda.  

Elias Pelembe aliiandikia Msumbiji bao la pili dakika ya 81 kwa shuti la mpira wa adhabu lililotinga nyavuni moja kwa moja, baada ya yeye mwenyewe kuangushwa nje kidogo ya eneo la hatari na Kevin Yondan.

Stars ilianzisha mpira haraka na kuendelea kusaka mabao, lakini bado Batte aliendelea kikwazo kwao- kwa kuwabeba wenyeji.

Baada ya Mganda huyo kupuliza kipyenga cha kumaliza mchezo, wachezaji wa Stars walimfuata kumlalamikia huku wakilia kwa kuwanyonga wazi wazi leo. 

Wachezaji wa Stars walishindwa kuificha huzuni yao baada ya kuanza kulia uwanjani kwa matokeo hayo, hali ilikuwa mbaya zaidi kwa Thomas Ulimwengu na Shomary Kapombe ambao walikuwa hoi baada ya kulia sana.

Stars ambayo mara ya kwanza na ya mwisho ilicheza AFCON mwaka 1980 enzi hizo bado ikiitwa Kombe la Mataifa Huru ya Afrika, sasa itasubiri mbio za kuwania fainali za michuano hiyo za mwaka 2017 nchini Libya.

Kikosi cha Stars kilikuwa; Deo Munishi ‘Dida’, Said Mourad, Shomary Kapombe, Kevin Yondan, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Erasto Nyoni, Thomas Ulimwengu/Mrisho Ngassa dk75, Mwinyi Kazimoto, John Bocco/Simon Msuva dk65, Mbwana Samatta na Khamis Mcha ‘Vialli’/Amri Kiemba dk46.

Msumbiji; Dario Khan, Momed Hagi, Zainadine Junior, Saddan Guambe/Eduardo Jumisse dk80, Francisco Mioche, Elias Pelembe/Isaac de Carvalho, Josemar Machaisse, Reginaldo Fait, Apson Manjate/Clesio Bauque dk41, Almiro Lobo na Richard Campos.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 19575

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>