Watuhumiwa ambao ni viongozi wa Chuo cha IMTU wakiwa chini ya ulinzi baada ya kufikishwa katika kituo cha Polisi Osterbay jijini Dar es Salaam.
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.
Wakati ikibainika kuwa viungo vya miili ya binadamu vilivyookotwa juzi katika Bonde la Mto Mpiji nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam vilitoka katika Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Tiba na Teknolojia (IMTU), jana Jeshi la Polisi liliwatia nguvuni watumishi wanane wa chuo hicho kuhusiana na sakata hilo.
Kukamatwa kwa watumishi hao kumeelezwa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova kuwa ni baada ya uchunguzi wa awali kubaini kuwa viungo hivyo kwa mara ya mwisho vilikuwa katika maabara ya IMTU.
Alisema tukio hilo lilitokea juzi jioni eneo la Bonde la Mbweni Mpiji ambako iligundulika mifuko ya plastiki 85 yenye mabaki ya viungo vya binadamu.
Kutokana na tukio hilo, Polisi imeunda jopo la wapelelezi saba likiongozwa na Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu, Jafari Mohamed kusaidiana na daktari wa jeshi hilo kufanya uchunguzi wa miili hiyo.
“Katika uchunguzi wetu tulibaini kuwa hivyo viungo vya binadamu vilitolewa katika Chuo cha IMTU na kusindikizwa na mfanyakazi wa ngazi ya juu kwa ajili ya kutupwa eneo la Bonde la Mbweni Mpiji,” alisema Kova.
Alisema mifuko hiyo ilikuwa myeusi ikiwa na viungo vya aina mbalimbali vikiwamo vichwa, miguu, mikono, moyo, mapafu, vifua na mifupa ya aina mbalimbali.
“Viungo hivyo havikuwa na harufu wala uvundo wa aina yoyote na vilionekana vimekaushwa na kukakamaa,” alisema.
Alisema katika eneo hilo walikuta vifaa vinavyotumika hospitali kama glovu, nguo maalumu (apron) 20 na karatasi mbili zenye maswali ya kujibu.
Kova alisema viungo hivyo vilichukuliwa na kupelekwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).