Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.
MWIMBAJI wa Hip Hop, Emmanuel Elbariki maarufu kama Ney wa Mitego, amesema wimbo wake wa ‘Nakula Ujana’ unampa raha kutokana na kupokewa kwa shangwe na mashabiki wa kizazi kipya nchini.
Msanii Ney wa Mitego pichani.
Ney wa Mitego aliyasema hayo katika mazungumzo ya kuelezea namna gani amejiwekea mikakati ya kulinda hadhi na uwezo wake kisanaa jijini Dar es Salaam, ikiwa ni siku chache baada ya kuwapa raha wakazi wa Mji wa Moshi katika Uzinduzi wa Tamasha la Kilimanjaro Music Tour 2014 lililofanyika katika Uwanja wa Ushirika.
Alisema kuwa wimbo wake huo wa Nakula Ujana umetokea kupendwa na wengi, hasa anapokuwa katika maonyesho mbalimbali, hivyo kuonyesha kuwa maendeleo yake kisanaa yamekuwa mazuri kupita kiasi.
“Nawashukuru wadau wangu wote kwakuwa wanapenda kazi zangu, hasa huu wimbo wa Nakula Ujana, ambao mimi mwenye unanipa raha.
“Naamini kila kitu kitakuwa kizuri zaidi kwa kuwapatia raha mashabiki wangu wakati wowote, kwakuwa bado nitaendelea kupambana ili kufanya vizuri zaidi katika tasnia ya muziki wa kizazi kipya nchini,” alisema.