BONDIA Ronald Pontillas, atawasili nchini leo kwa ajili ya pambano lake la kimataifa dhidi ya bondia Francis Miyeyusho, litakalofanyika Jumamosi kwenye Ukumbi wa PTA, Dar es Salaam.
Akizungumza Dar es Salaam jana, mratibu wa pambano hilo Mussa Kova, alisema kuwa Pontillas raia wa Ufilipino, atawasili nchini akiwa na kocha wake Amogo Samson.
Kova alisema bondia huyo atawasili majira ya saa moja asubuhi, akitumia ndege ya Qatar Airways.
Alisema kuwa moja kwa moja ataenda hotelini kupomzika kabla ya saa 5, kuzungumza na vyombo vya habari.
Kova alisema kuwa maandalizi mengine yanaendelea vizuri ambapo, hata suala la viingilio nalo tayari limeshapangwa.
Alisema katika viingilio vitakuwa vya aina mbili ambavyo ni sh.20,000 kwa VIP na kawaida itakuwa sh.10,000.
Alisema kuwa katika pambano hilo kutakuwa na mapambano ya utangulizi ambayo atayatangaza kesho katika mkutano maalum na vyombo vya habari.
Pia Kova alisema maandalizi yanakwenda vizuri na kusisitiza kuwa litasimamiwa na chama cha ngumi za kulipwa Tanzania (PST).
"Mabondia wote wako katika hali nzuri ya ushindani, tunategemea Miyeyusho atafanya vizuri na kukabiliana na upinzani wa mpinzani wake kwani ni bondia mzuri na mwenye kiwango cha juu," alisema Kova.