Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu Bi. Joyce Fisoo akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) katika ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo jijini Dar es Salaam katika kuelezea mafanikio ya bodi ya filamu nchini tokea imeanzishwa. Kushoto ni Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bi. Consilia Niyibitanga.
Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu Bi. Joyce Fisoo akionyesha moja ya picha zinazotolewa na wadau wa filamu kama matangazo ya kutambulisha filamu zao sokoni, kushoto ni Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bi. Consilia Niyibitanga. Picha zote na Cathbert Kajuna wa Kajunason Blog.
---
Na Mwandishi Wetu.
Serikali imesema inatambua Tasnia ya Filamu ikiendelezwa vizuri ni chanzo kikubwa cha ajira kwa vijana na ni njia madhubuti ya kukuza uchumi kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.
Kauli hiyo imetolewa leo na Mkuu wa kitenngo cha mawasilianao serikalini Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Concilia Niyibitanga wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliofanyikia ukumbi wa Idara ya habari Maelezo jijini Dar es Salaam.
Bi. Concilia alisema kuwa mwamko unaongezeka kwa wasanii na watengenezaji wa filamu kutoka ndani na nje ya nchi. Hii inajidhihirisha kwa idadi ya vibali vya utengenezaji filamu imeongezeka kutoka 100 mwaka 2000 hadi 472 Januari 2014.
Aidha, kampuni zinazojishughulisha na uendeshaji wa shughuli za filamu nchini zimeongezeka kutoka Kampuni moja ya Filamu Tanzania (TFC) na kufikia 129 mwaka 2013 na upande wa watengenezaji wa filamu za ndani, uwasilishaji wa ukaguzi umeongezeka kutoka filamu 96 mwaka 2000 hadi kufikia 1059 Februari 2014.
Naye Katibu Mtendaji wa Bodi ya filamu nchini Joyce Fisoo alitoa rai kwa wasanii wa filamu kutumia lugha ya Kiswahili hasa katika uandaaji wa jina ili kulinda na kuikuza lugha yetu ya Kiswahi.
Tasnia ya Filamu nchini ilianza tangu mwaka 1920 wakati wa ukoloni, baada ya Uhuru, Serikali ya Tanzania kupitia bunge iliamua kutunga sheria namba 4 ya mwaka 1976 ya Filamu na Michezo ya kuigiza ili kuweka usimamizi mzuri wa tasnia hiyo.