Na Veronica Kazimoto - MAELEZO
Ofisi ya Taifa ya Takwimu imetoa wito kwa viongozi mbalimbali wakiwemo wanasiasa wote nchini kutumia taakwimu sahihi zinazotolewa na Ofisi hiyo ili ziweze kutumika katika kupanga mipango mbalimbali ya maendeleo.
Akizungumza na mwandishi wa habari hii jijini Dar es Salaam, Meneja wa Teknojia ya habari na Masoko Bi. Mwanaidi Mahiza amesema Ofisi ya Takwimu imerahisisha upatikanaji wa takwimu hizo kupitia Kanzidata inayoonesha viashiria vya kiuchumi na kijamii (Tanzania Social Economic Database -TSED).
“Lengo la kanzidata hii sio kuzibana Wizara wala kuwashurutisha wanasiasa kutumia takwimu bali ni kuwarahisishia watumiaji wote wa takwimu kupata taarifa kwa wakati pindi wanapokuwa katika kazi zao za kila siku,” amesema Bi. Mahiza.
Meneja huyo amefafanua kuwa TSED inasaidia kuondoa mlolongo wa upatikanaji wa taarifa uliopo kwenye baadhi ya ofisi nyingi ambapo wakati mwingine mteja huambiwa aaandike barua au arudi baada ya siku kadhaa.
Aidha, amesisita kuwa ni muhimu kutumia Kanzidata hiyo kwa kuwa ndani yake kuna takwimu rasmi ambazo zinatoka katika vyanzo sahihi vyenye mamlaka ya kutoa takwimu hizo hapa nchini.
Bi. Mwanaidi Mahiza ameyasema hayo wakati akikanusha habari iliyoandikwa na moja ya gazeti la kila siku lililoripoti kuwa Ofisi ya Taifa ya Takwimu kupitia marekebisho ya sheria ya takwimu ya mwaka 2002 ambayo yako bungeni kutumika kuzibana wizara ili zitoe takwimu sahihi katika ripoti zao kitu ambacho hakikuzungumzwa.
Hivi karibuni baadhi ya wahariri na waandishi wa habari walipewa mafunzo na Ofisi ya Taifa ya Takwimu juu ya Kanzidata inayoonesha viashiria vya kiuchumi na kijamii (Tanzania Social Economic Database -TSED) ambapo baadae moja ya gazeti la kila siku liliandika habari yenye kichwa cha habari Ofisi ya Takwimu kuzibana wizara.
Kanzidata inayoonesha viashiria vya kiuchumi na kijamii ilizinduliwa rasmi mwaka 2001 ikiwa na viashiria 75 ambapo hivi sasa ina viashiria 940 na inapatikana katika mfumo wa DVD, CD ROMs na tovuti ya www.tsed.org.