Nipo Dodoma kufanya kazi kubwa na ya muhimu kwa mustakabali wa taifa letu tukufu. Kazi ya kutengeneza katiba ambayo kama ikipitishwa na wananchi, basi ndio itakuwa katiba mpya ya Tanzania.
Ni kazi ya siku 70, zikizidi sana ni siku 90. Ni siku zitakazobadilisha kabisa maisha yangu, kwani nitaingia kwenye historia ya kushiriki kuandika katiba ya nchi yetu.
Kwangu mimi hayo ni malipo tosha kwani najivunia kuteuliwa na Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete kuwa moja kati ya watu wachache watakaoshiriki kwa karibu kabisa kufanya kazi hii ambayo inaweza isifanyike tena kwa miaka 50 hata 100 ijayo!
Sitegemei kutajirika kwa kazi hii kwani kwa kushiriki tu, ni utajiri tosha kwenye maisha yangu, hivyo kama ni hela ya kujikimu, posho 300,000/- inanitosha sana, sana, sana! Hivyo basi napinga bila wasiwasi wala shaka lolote ombi la ongezeko la posho kwa wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba, kwani kuwa miongoni mwa Watanzania wachache katika Bunge hili nimalipo makubwa kuliko 300,000/=
Pamoja na hayo nawasii wajumbe wenzangu tufanye kazi hii ya kihistoria kwa moyo mkunjufu umakini na uadilifu mkubwa kwa niaba ya wananchi wenzetu. Kwa pamoja tutaweza bila posho ya nyongeza.