NA OSCAR ASSENGA, MUHEZA.
MKUU wa Mkoa wa Tanga, Luteni Kanali Mstaafu, Chiku Gallawa amewataka wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani hapa kuacha kujiingiza kwenye mapenzi wakiwa mashuleni kwani hali hiyo itawafanya kushindwa kufikia malengo yao.
Gallawa alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na wanafunzi wa shule ya sekondari ya Potwe kwenye ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo,kusikiliza kero za wanannchi kupitia mikutano ya hadhara kwenye kata na vijiji mbalimbali wilayani hapa.
Alisema wanapaswa kutumia vizuri muda wao wakiwa shuleni kwa kujisomea kwa bidii ikiwemo kupenda masomo ya sayansi ili waweze kuongeza kasi ya wataalamu wa masomo hayo kwa siku zijazo kitendo ambacho kitaongeza hamasa ya wenzao wengine.
"Hakikisheni mnatumia vizuri muda wenu kwa kusoma kwa bidii kwani hiyo ndio silaha pekee ambazo itawainua kimaisha na kuwakwamua na umaskini walionao kwenye jamii zenu na Taifa kwa ujumla ikiwemo kuacha kujiingiza kwenye mapenzi 'Alisema RC Gallawa.
Akizungumzia suala la upandaji wa miti,Mkuu huyo wa mkoa aliagiza vitalu vya miti kwa shule za msingi na sekondari kuhakikisha wanapanda miti ipatayo 4000 ili kusaidia kuepukana na ukosefu wa mvua na uharibifu unaosababishwa na upepo mkali.
Awali akizungumza kabla ya kumkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mkuu wa wilaya ya Muheza, Subira Mgalu alisema wilaya hiyo imeanzisha msako maalumu wa kusaka wazazi ambao hawajawapeleka watoto wao shuleni waliofaulu.
Mgalu alisema ikibainika wanafunzi hao wameozeshwa wazazi watachukuliwa hatua kali ikiwmo kufikishwa kwenye vyombo vya sheria ili kuweza kukomesha vitendo vya aina hiyo wilayani humo.
"Mh.Mkuu wa Mkoa Tumeweka utaratibu wa kutoza faini ya sh.elfu moja kwa wanafunzi watoro ambapo fedha hizo huhesabiwa kwa kila siku aliokosa na hupelekwa kwenye uchangiaji wa ujenzi wa maabara "Alisema DC Mgalu.