Timu ya Tanzania ya wasichana chini ya umri wa miaka 17 ya Airtel Rising Stars juzi, jumanne imeifunga Sierra-Leone magoli 2-1 katika mechi yao ya kwanza ya kimataifa iliopigwa katika jiji la Lagos ,Nigeria.
Baada ya kuwashuhudia kaka zao wakilala kwa goli 2-1 dhidi ya Ghana juzi asubuhi ,timu ya wasichana walianza kwa kasi na kupata nafasi nyingi za kufunga lakini walinzi wa Sierra Leone walikua makini na kuondosha mipira yote katika eneo la hatari. Iliwachukua dakika 20 kwa Sierra-Leone kupata goli la kuongoza kupitia kwa Fatimata..
Timu ya Tanzania walionyesha uhai wakitafuta goli la kusawazisha, juhudi zao zilizaa matunda na kusawazisha bao katika dakika ya 27 baada ya Vumilia Maarifa kuunganisha pasi nzuri kutoka winga wa kulia.
Dakika sita kabla ya kwenda mapumziko, Tanzania walipata goli la kuongoza kupitia kwa mshambuliaji mwenye kasi Neema Paul ,aliefunga goli muhimu na kuwapa point tatu zilizowaletea matumaini ya kuchukua ubingwa.
Akiongea kuhusu timu ya wavulana iliopoteza mchezo wao kwanza kocha Abel Mtweve amesema timu imekosa uzoefu na mabeki kutokua makini, ila ameahidi atalishughulikia swala hilo na wataibuka na ushindi dhidi ya Zambia.
Naodha wa timu ya Wavulana , Thomas Chindeka amesema kuwa , “ mechi ilikua nzuri , tulikua wa kwanza kupata goli lakini hatukuweza kulinda goli letu . Ni wageni kwenye mashindano haya , tumekuja jana na tunatakiwa kufanya mazoezi vizuri na kuzoea mazingira. Ili tuna imani tutafanya vizuri mchezo unaofata” .
Timu ya wasichana baada ya kuibuka na ushindi dhidi ya Sierra-Leone watacheza na Uganda siku ya jumatano tarehe 18 kabla hawajakutana na Malawi Alhamisi tarehe 19 septemba. Mashindano yataingia hatua ya mtoano ijumaa na fainali itapigwa jumapili tarehe 22 septemba.
Washindi wote wavulana na wasichana watapata zawadi ya dola za marekani 10,000 kwa ajili ya elimu ya wachezaji. Mchzaji wa zamani wa kimataifa na timu ya Arsenal ya Uingereza Robert Pires anatarajiwa kuwasili jijini Lagos tarehe 21 septemba ambapo atakua mgeni rasmi katika fainali.