Vijkundi vya Ulinzi Shirikishi wilaya ya Handeni mkoani Tanga, vimemuomba Mkurugrnzi wa wilaya hiyo kuwasaidia kupata ofisi na vitendea kazi muhimu ili viwawezeshe kutekeleza wajibu wao kikamilifu.
Ombi hilo limetolewa jana na Mkuu wa Vikundi vya Ulinzi Shirikishi wilaya ya Handeni Bw. Richard Matula, wakati akizungumza na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Handeni Bw. Thomas Mzinga.
Bw. Matula, alisema kuwa kama Halmashari itajitahidi kuwapatia vijana hao vitendea kazi na ofisi ya kufaa, ni wazi kuwa vikundi hivyo vitaweza kufanya kazi zao kwa uhakika zaidi na kudumisha hali ya ulinzi na usalama katika mji huo.
Alisema kuwa sio busara kazi ya kuvilea vikundi hivyo ikabaki mikononi mwa Polisi pekeee kwa sababu suala la Ulinzi na Usalama ni jukumu la kila mmoja wetu wakiwemo viongozi wa Serikali na wa Halmashauri za mini na Vijijii.
Bw. Matula, ameyataja baadhi ya mahitaji muhimu kwa vijana wake kuwa ni tochi, betrii, filimbi, makoti ya mvua, viatu aina ya boot na virungu.
Hata hivyo akijibu hoja hizo, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya mji wa Handeni, Bw. Thomas Mzinga, alisema kuwa anakubaliana na maombi hayo na kwamba ofisi yake itayapa umuhimu mkubwa kwa lengo la kudumisha hali ya usalama wa mjini huo.
Amesema bila ya usalama wa kutosha hakutakuwa na uzalishaji mali ama hata zikizalishwa kinachopatikana huporwa na wahali, hivyo ameona ipo haja ya kuviimarisha vikundi vya Polisi jamii na Ulinzi Shirikishi ili kudumisha hali ya utulivu na usalama wa mjini wa handeni Chanika.
Bw. Mzinga amekubali kuwapatia Ofisi na kuvisajili vikundi mbalimbali vya ulinzi shirikishi wilayani humo na hata kuvifungulia akauti benki ili mapati yanayopatikana kwa ajili ya ulinzi zihifadhiwe benki.
Alikiri wazi kuwa kuwepo kwa vikundi vya Ulinzi Shirikishi katika mji huo, kumesaidia kwa kiasi kikubwa katika kuuweka mji huo katika hali ya usalama na kwamba tangu kuanzishwa kwa vikundi hivyo, kumeufanya mji wa Handeni kutokuwa na matukio mengi ya kihalifu.
Aidha Bw. Mzinga ameahidi kushirikiana na watadau mbalimbali wakiwemo wafanyabiashara wa mji huo ili kuviwezesha kimaslahi Vikundi hivyo vya Ulinzi Shirikishi.
Hivi karibuni Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Handeni SP Zuberi Chembera, alitoa msaada wa tochi na filimbi kwa vikundi kadhaa vya ulinzi Shirikishi wilayani humo misaada ambayo pia ilitolewa na baadhi ya wafanyabiashara wilayani humo.