(Na Belinda Kweka - MAELEZO)Dar es Salaam
Serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imefanya jitihada katika kuimarisha na kuboresha huduma za afya kwa kuongeza watumishi wa kada za afya nchini.
Akizungumza na Waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Msemaji wa Wizara hiyo Nsachris Mwamwaja, amesema kuwa Wizara imepiga hatua katika kuimarisha, kuboresha na kusambaza huduma za afya na ustawi wa jamii kwa kuongeza ajira za watumishi katika kada mbalimbali za afya nchini.
“Hivi sasa Serikali inajitahidi kukabiliana na suala la upungufu wa watumishi wa kada za afya kwa kuongeza ajira na kuwapangia wataalam wenye sifa katika vituo vya kutolea huduma”, alisema Mwamwaja.
Aidha amesema kuwa katika mwaka wa fedha 2012/2013 Wizara ilipata kibali cha kuwapangia vituo vya kufanyia kazi wataalam 8,869 kwa ajili ya mamlaka mbalimbali za ajira ikiwemo Taasisi ya Saratani Ocean Road, Hospitali ya Taifa Muhimbili na nyinginezo.
Aliongeza kuwa baada ya kukuza mpango huo pia Wizara iliweza kudahili wanafunzi wengi ili kuweza kukabiliana na upungufu wa watumishi wa kada za afya ambapo kuanzia mwaka 2009 hadi mwaka huu wameweza kudahili wanafunzi 27,492 na kuajiri 28,360 katika kipindi cha mwaka 2008 hadi 2012.
“Kwa kiasi kikubwa Serikali inajitahidi kuboresha huduma za afya na mpaka sasa tunaendelea kupata taarifa kutoka mikoa mbalimbali kuhusu watumishi wetu kuripoti vizuri katika vituo vyao na kutoa huduma ipasavyo” aliongeza Mwamwaja.
Nsachris Mwamwaja amewakumbusha watumishi wa kada ya afya waliopangwa katika vituo mbalimbali kulipoti moja kwa moja kwa mamlaka ya ajira zao pamoja na viambatanisho vyao vyote.