Wananchi wakivuka kwa miguu katika Daraja la Manung’una, lililopo katika Kijiji cha Msisi, Singida ambalo limekatika kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha.
MVUA zinazoendelea kunyesha mkoani Singida, zimesababisha maafa makubwa baada ya watu wawili, mmoja akiwa raia ya China, kufariki dunia kwa kusombwa na maji, huku mamia ya abiria wakikwama njiani baada ya daraja linalounganisha mkoa huo na mingine kukatika. Kukatika kwa Daraja la Munung’una kwa siku mbili sasa, kumesababisha msongamano mkubwa wa magari yanayokadiriwa kuwa zaidi ya 300.
Habari zilizopatikana jana zimeeleza kuwa waliofariki dunia kutokana na mvua hizo ni Xue Hui (36), maarufu kwa jina la Kevin na Mariamu Samweli (18), mkazi wa Kijiji cha Maluga ambao walifariki dunia kwa nyakati tofauti baada ya kusombwa na maji.
Vifo vyao vimeongeza idadi ya watu waliofariki dunia kutokana na mvua mkoani Singida kufikia sita katika siku tatu zilizopita. Mvua za juzi, zilisababisha watu wanne wa familia moja katika Wilaya ya Mkalama kupoteza maisha baada ya kuangukiwa na nyumba ya tembe.
Mkuu wa Wilaya hiyo, Edward Ole Lenga alisema raia huyo wa China, alifariki dunia juzi jioni katika Kijiji cha Gumanga Wilaya ya Mkalama baada ya gari alilokuwa anasafiria kusombwa na maji... “Mchina huo alikuwa na mtoto wake ambaye alinusurika kifo.”
Alisema Mariamu alifariki dunia baada ya kusombwa na maji katika Mto Kiula uliopo katika Kijiji cha Igonia. “Miili ya marehemu hao imehifadhiwa kwenye chumba cha maiti cha Hospitali ya Mkoa wa Singida.”
Abiria wakwama Mvua hizo kubwa zilizonyesha tangu mwishoni mwa Desemba mwaka jana, zilisababisha daraja hilo la Munung’una lililopo katika Kijiji cha Msisi wilayani Singida kuvunjika.
Kutokana na athari hiyo, kumekuwa na msongamano mkubwa wa magari baada ya mawasiliano kati ya Singida na mikoa ya kanda ya ziwa na nchi jirani kukatika.
Baadhi ya wananchi walilalamikia uharibifu huo wakisema umetokana na ujenzi wa daraja hilo kuwa wa kiwango cha chini.
Dereva, George Medadi akitokea Mwanza kwenda Dar es Salaam, alisema
daraja hilo limechangiwa kwa kiasi kikubwa na kujengwa chini ya kiwango.