Habari zilizofikia toka Mtwara na kudondokea dawati letu la habari Kajunason Blog, hali ya mji wa Mtwara bado si shwari ambapo mpaka sasa nyumba kadhaa za wananchi, vibanda vya biashara katika eneo la Mgomeni zimeteketezwa kwa moto tokea asubuhi na nyingine zinaendelea kuteketea.
Kwa mujibu wa mwandishi wetu aliyepo eneo la tukio anasema hali bado tete huduma za kijamii katika mji huo zimesimama zikiwemo usafiri, huduma za kibenki na shule huku wasafiri kutoka jijini Dar es Salaam wakidaiwa kukwama katika eneo la usijute wakihofia kuingia mjini humo.
Taarifa za polisi zinasema kuwa mpaka sasa jumla ya watu 91 wamekamatwa huku wengine wakiendelea kukamatwa katika maeneo mbalimbali ya mji huo. Kwa habari zaidi kuhusiana na vurugu hizo endelea kuunga nasi.
RIPOTI TOKA KWA BARAKA UFUNGUO, MTWARA.
-Mwanafunzi wa CHUNO afikishwa hospitali Ligula na majeraha ya risasi mguuni.
-Maduka maeneo ya Magomeni yamechomwa moto ikiwamo pia mali za Askari magereza na uhalifu ukifanyika vidole vinawaelekea Polisi.
-Afisa Usalama wa Taifa ambaye anamiliki nyumba ya wageni naye amevamiwa na kuporwa mali ikiwamo fedha katika gesti yake. Haijajulikana ni kiasi gani cha mali kilichopotea.
-Mabomu yanaendelea kupigwa tofauti kwa sasa hayapigwa mfululizo.
Mabomu yametulia. Hali ya ukimya imetawala.
-Mabasi 5 ya Champion yamebeba Wanajeshi yako njiani yanakuja.
Serikali yatoa tamko yasema watu 91 wanashikiliwa.
-Bunge laahirishwa tena. Kupisha uchunguzi na kuepusha uchochezi kutoka kwa baadhi ya wabunge. (Kwa mujibu wa Spika).
-Maeneo ya Magomeni, Chikongola, Nkanaledi, Mikindani maaskari wanaingia majumbani mwa watu na kumsomba mtu yeyote ambaye ni mwanaume awe amehusika awe hajahusika na kumkamata. Pia inaripotiwa na uhalifu unafanywa na maaskari hao hao. Jambo linaloamsha hisia kwa wananchi.
-RPC anaongea na vyombo vya habari na kuwasihi wananchi waende makazini. Lakini kiuhalisia hali sio shwari.
-Mahakama ya mwanzo ya Mitengo imechomwa moto, mpaka sasa ni vita baina ya wananchi na maaskari. Mabomu yamesikika pamoja na milio ya risasi masaa 24. Na milio ya Risasi na mabomu inaendelea kusikika.
-Raia wapatao 7 wameripotiwa kufariki (wengine walipelekwa hospitali ya Ndanda Ndogo na mmoja ameripotiwa kupokelewa Ligula.
-Nyumba za viongozi zinaendelea kuchomwa moto, Majibizano baina ya Polisi na Raia yanaendelea maeneo ya Magomeni, Nkanaledi na Mikindani.
-Maduka yamefungwa na hakuna huduma zozote
-Barabara zimewekwa vizuizi magogo na matairi yamechomwa moto. Hakuna njia ya kupita.