Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Viwanda na Biashara, wakiangalia uzalishaji walipotembelea kiwanda cha Konyagi cha Tanzania Distilleries Limited (TDL), Dar es Salaam hivi karibuni.
---
Na Mwandishi Wetu.
BAADHI ya wananchi jijini Dar es Salaam, wamelalamikia hoja iliyozuka bungeni wiki hii kwamba kinywaji cha Konyagi aina ya Kiroba kipigwe marufuku nchini.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi hao, walisema endapo serikali itachukua uamuzi wa kupiga marufuku kinywaji hicho, watarudia kunywa pombe aina ya gongo ambayo ni hatari kwa afya zao.
Mkazi wa Mbagala, Faustine Mwiruka aliyekutwa kwenye baa ya Kisuma, aliiasa Serikali kutothubutu kukubali kinywaji hicho kupigwa marufuku, kwani ikifanya hivyo wengi wa wananchi wenye kipato cha chini wataanza tena kunywa gongo na pombe za kienyeji.
Itabidi tufanye kama Zambia ambao wamezuia viroba, lakini nchi nzima imejaa viroba vya Malawi, Zaire na Burundi, lazima tuiadhibu serikali ikose kodi kote kote, bia hatunywi, viroba vya nje tutakunywa, pamoja na gongo.
Alisema haingii akilini kukihusisha kinywaji hicho na ajali za magari, akidai kuwa hata kabla ya viroba kuingia sokoni ajali zilikuwepo nyingi.
"Sisi tuna imani na viroba kwa vile vina ubora wa uhakika tofauti na pombe ya gongo ambayo inapikwa bila kupimwa ubora hivyo ni hatari kwa usalama wa afya zetu." alisema Mwiruka.