Mheshimiwa Angellah Kairuki (MB), Naibu Waziri wa Katiba na Sheria akiwa na mwenyeji wake Mhe. Sayid Ashraful Islam, Waziri wa Serikali za Mitaa Maendeleo Vijijini na Ushirika, (Wizara inayoshughulika na Usajili wa Vizazi na Vifo) wakati wa ziara yake nchini Bangladesh kujifunza namna ambavyo nchi hiyo imeweza kufikia asilimia zaidi ya 95 ya usajili wa Vizazi na Vifo.
Mhe. Angellah Kairuki akielezwa jambo na Bw. Nazrul Islam, Mtendaji Mkuu wa Dhaka South City Corporation
Mheshimiwa Angellah Kairuki akifafanua jambo kwa Mhe. Mhe. Hassanul Haq Inu, Waziri wa Habari wa Bangladesh wakati wawili hao walipokuwa wakisubiri kukutana na waandishi wa habari wa Bangladesh na kueleza madhumuni ya ujumbe wa Tanzania kwenda nchini Bangladesh kujifunza namna ya kuboresha mfumo wa usajili wa vizazi na vifo hadi kufikia asilimia mia moja (100%).
Mhe. Angellah Kairuki akiwa katika picha ya pamoja na ujumbe wake wa wataalam kutoka Taasisi za RITA, NIDA, TRA, Serikali za Mitaa, e-Government, Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Ofisi ya Takwimu, Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Wenyeji wake.
Mheshimiwa Angellah Kairuki, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria akijibu baadhi ya maswali ya waandishi wa habari wa Bangladesh
Mhe. Angellah Kairuki katika picha ya pamoja na Sir. Fazle Abed, Mwanzilishi na Mwenyekiti wa taasisi ya BRAC alipotembelea Makao Makuu ya BRAC.
USAJILI WA VIZAZI NA VIFO NCHINI
---
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mheshimiwa Angellah Kairuki aliongoza ujumbe wa Tanzania kwenda nchini Bangladesh tarehe 5-11 Aprili 2013. Ujumbe huo uliojumuisha wataalam kutoka taasisi mbalimbali za Serikali zinazojihusiha na masuala ya usajili ikiwa ni pamoja na RITA, NIDA, TRA, Serikali za Mitaa, e-Government, Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Ofisi ya Takwimu ulikwenda kujifunza namna ambavyo nchi ya Bangladesh ilivyoweza kufanikiwa katika zoezi la Usajili wa Vizazi na Vifo kwa zaidi ya asilimia 95 ya wananchi wao.
Katika ziara hiyo Mheshimiwa Naibu Waziri na ujumbe wake walijionea jinsi ambavyo zaidi ya huduma 16 muhimu nchini Bangladesh zilivyounganishwa na Mfumo wa kusajili vizazi na vifo na umuhimu wa cheti cha kuzaliwa. Huduma hizo ni pamoja na Vitambulisho vya Taifa, Leseni ya Biashara, Kitambulisho cha mlipa Kodi (TIN), leseni ya kuendesha gari, hati ya kusafiria, leseni ya ukandarasi, vibali vya ujenzi, leseni ya kusafirisha na kuagiza bidhaa ndani na nje ya nchi, kuunganishiwa huduma muhimu kama umeme, maji, simu n.k. bila kuwa na cheti cha kuzaliwa mwananchi wa Bangladesh hawezi kupata huduma mojawapo kati ya hizo.
Serikali kwa kutambua umuhimu na faida za kusajili vizazi na vifo, imedhamiria kuboresha mfumo wa Usajili na kunyanyua kiwango cha Usajili kwa kuanzisha Mpango wa Usajili wa Watoto wote walio na umri chini ya Miaka Mitano (Under Five Birth Registration Initiative(U5BRI) na mpango wa usajili wa watoto wenye umri wa miaka 6-18.
Katika mpango huu wa Usajili, mtoto atasajiliwa na kupatiwa cheti papo hapo, na hivyo kufanya zoezi zima la usajili kuwa la hatua moja badala ya hatua mbili zinazotumika sasa, yaani kusajili kwanza kisha kupata cheti baadaye. Pia Mpango huu una lengo la kugatua madaraka ya shughuli za usajili kutoa Serikali Kuu na kupeleka katika Serikali za Mitaa na Vituo vya Afya.