Quantcast
Channel: HABARI NA MATUKIO
Viewing all articles
Browse latest Browse all 19575

MNYIKA AHAIDI KUMSOMESHA MWANAFUNZI BORA CHUO CHA JINSIA

$
0
0
Na Joachim Mushi

MBUNGE wa Jimbo la Ubungo kupitia tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Mnyika (PICHANI) ameahidi kumsomesha mwanafunzi bora wa Chuo cha Jinsia (GTI) kupitia sehemu ya mshahara wake wa ubunge.
Mbunge huyo alitoa ahadi hiyo jana jijini Dar es Salaam katika sherehe za Mahafali ya Kwanza ya Chuo cha Jinsia, GTI alipokuwa mgeni rasmi. Alisema anatambua mchango wa chuo hicho katika kuiandaa jamii kupigania usawa wa rasilimali za taifa, hivyo kupitia mshahara wake wa ubunge atatoa mchango wa kumlipia ada mwanafunzi bora wa chuo hicho mwakani.

Mbunge huyo aliupongeza uongozi wa GTI kwa mafanikio waliofikia ya kuanzisha chuo kinachotoa mafunzo ya jinsia kwa jamii na kushauri uongozi kujipanga na kuwasilisha ombi la kuomba fungu la fedha kutoka Mfuko wa Mbunge wa Maendeleo wa Jimbo ili kukiwezesha chuo hicho kufanya shughuli zake kiufanisi.
Awali akizungumza katika mahafali hayo, Mkuu wa Chuo cha GTI, Dk. Diana-Bupe Mwiru alisema mahafali hayo ni ya kihistoria kutokana na kwamba yanafanyika kipindi ambacho Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) ambao ni wamiliki wa chuo hicho wakisherehekea miaka 20 tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo.

"TGNP inasherehekea miaka 20 ya harakati za ukombozi wa mwanamke kimapinduzi dai kuu likiwa rasilimali za nchi kunufaisha watu wote na hasa wale walioko pembezoni. Mwanamke wa kitanzania amekuwa miongoni mwa makundi yaliyoko pembezoni kutokana na mila na sheria kandamizi ambazo zilishindwa kutambua mchango wa mwanamke katika jamii na majukumu makubwa ambayo ameyabeba ili kuhakikisha kuwa jamii inaendelea kuwepo," alisema Dk. Mwiru.
Aliongeza kuwa GTI tangu kuanzishwa kwake imekuwa ikitoa mafunzo kwa umahiri mkubwa katika soko la ndani na nchi za jirani, huku kikiwa kimefundisha washiriki zaidi ya 6000 kutoka nchi za Msumbiji, Nigeria, Malawi, zambia, Kenya, Rwanda, Uganda, Ethiopia, Norway pamoja na Tanzania yenyewe.

Jumla ya wahitimu wa 11 walifanikiwa kutunukiwa vyeti vya mafunzo ya jinsia katika mahafali hayo ya kwanza.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 19575

Trending Articles