Mhe. Naibu Spika Job Ndugai akipokea Nishani hiyo kutoka kwa Dkt. Mohammed Zaharani. Wakiangalia kwa furaha ni Mhe. Beatrice Shelukindo, Bi Mariam Mungula na Bw. Haruna Mbeyu. |
Mke wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambae pia ni Mwanaharakati wa Kijamii kupitia Chama Chake cha Wanawake na Maendeleleo, wiki iliyopita alizawadiwa Nishani na Chama kinachojishughulisha na kuinua kiwango cha Elimu kwa Nchi za Afrika Mashariki kilichoko katika jiji la London, Uingereza.
Akiongea katika Hafla hiyo fupi iliyofanyikia katika kumbi za Hoteli ya Park Plaza iliyopo pembeni mwa Westminster Bridge (katikati ya jiji la London) Dr Mohammed Zaharan ambae ni Katibu wa Chama hicho cha East Africa Education Foundation (EAEF) alisema kuwa Chama Chake kimekuwa kikifuatilia kwa ukaribu na shughuli zinazofanywa na Mama Kikwete kupitia Jumuiya ya WAMA na wamefurahi kupata fursa hii ya kumtunukia "Award" kwa mchango wake mkubwa sana wa kuinua Elimu ya Mtoto, hususan wa kike na vilevile kuwezesha Wanawake ili waweze kujitegemea. Dr Zaharani aliongeza kuwa Mama Kikwete ni mfano bora sana wa kuigwa na Wanawake katika jamii ndani na nje ya Tanzania.
Akipokea Nishani hiyo kwa Niaba ya Mama Salma Kikwete, Naibu Spika Mh. Job Ndugai (Ambae alikuwa Nchini Uingereza kwa Mualiko wa Naibu Spika wa Uingereza na aliongoza na Wabunge ambao ni Wajumbe wa Kamati ya Utumishi ya Bunge) alisema kuwa amefurahishwa sana na kitendo hicho cha Mchango wa Mama Salma kuonekana, kwa kuwa kinadhihirisha mchango unaofanywa na Jumuiya zisizo za Kiserikali katika jamii kama WAMA unaonekana mpaka Nje ya Tanzania.
Nae Mh. Mama Beatrice Shelukindo alifurahi zaidi kwa kitendo hiki na kusema kuwa hili ni jambo kubwa sana na linadhihirisha mchango mkubwa wa Mama Salma katika kumuendeleza Mwanamke wa KiTanzania na inatoa moyo kwa Wanawake Wengine.