Ndugu Wananchi;
Jambo la pili ninalotaka kuzungumzia ni ajali ya kuporomoka kwa jengo la ghorofa 16 lililokuwa linajengwa katika jiji la Dar es Salaam. Ajali hiyo iliyotokea juzi tarehe 29 Machi, 2013 imeleta msiba na simanzi kubwa nchini. Mpaka sasa maiti za ndugu zetu 36 zimepatikana. Watu 17 waliweza kuokolewa, wanne kati yao bado wanaendelea na matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Wengine walitibiwa na kuruhusiwa. Kazi ya kufukua eneo la ajali inaendelea na sasa inakaribia kufikia ukingoni.
Ndugu Wananchi;
Mimi na viongozi wenzangu tulipata nafasi ya kwenda kuangalia eneo la ajali. Hali niliyoiona pale imenihuzunisha sana. Lazima nikiri, hata hivyo, kwamba nimeridhishwa sana na juhudi kubwa za uokoaji zilizokuwa zinafanywa na wanajeshi wetu wakishirikiana na taasisi, mashirika binafsi na wananchi.
Napenda kutumia nafasi kutoa shukrani maalum kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Ndugu Saidi Meck Sadick kwa uongozi wake madhubuti. Pia nampongeza Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Ndugu Raymond Mushi, na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Ndugu Suleiman Kova pamoja na Maafisa na askari wa JWTZ, na wale wote walioshiriki na wanaoendelea kushiriki katika juhudi za uokoaji.
Nawapongeza pia madaktari na wauguzi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na hospitali nyinginezo kwa jitihada zao za kuokoa maisha ya waliojeruhiwa. Nawapa pole wale wote waliofiwa na wapendwa, ndugu na jamaa zao katika ajali hii. Nawaomba wawe na moyo wa subira huku sote tukiungana nao kuwaombea marehemu wetu wapate mapumziko mema peponi. Kwa waliojeruhiwa, tunawaombea wapone upesi.
Ndugu Wananchi;
Maneno mengi yanasemwa kuhusu chanzo cha ajali ile. Alimradi kila mtu ana dhana yake. Niliagiza vyombo na mamlaka husika wachukue hatua zipasazo kuchunguza sababu za ghorofa hilo kuanguka na watakaothibitika kusababisha maafa hayo wachukuliwe hatua zipasazo.
Wa kushtakiwa Mahakamani washitakiwe na wa kufutiwa leseni za kufanya shughuli za ujenzi au taaluma zao wafutiwe bila ajizi. Jambo la msingi la kusisitiza ni kuwa mamlaka zinazohusika na usimamizi wa ujenzi lazima zitimize ipasavyo wajibu wake. Naamini kama mamlaka hizo zingetimiza ipasavyo wajibu wake ajali hii ingeepukika. Halmashauri za miji na wilaya zina wajibu maalum kwenye ujenzi katika maeneo yao. Watimize wajibu wao. Yaliyotokea Dar es Salaam yawe fundisho kwa wote.
Ndugu Wananchi;
Kabla ya kumaliza hotuba yangu napenda kutumia nafasi hii kuwaomba na kuwasihi waandishi wa habari wasaidie kuliepusha taifa letu kuingia katika vita vya kidini. Waache kushabikia taarifa zinazochochea na kujenga uhasama baina ya waumini wa dini zetu. Nawaomba wapime athari za taarifa zao kabla ya kuziandika au kuzitangaza. Wawe makini na maneno wanayotumia. Katika hali tuliyonayo sasa lazima sote tuazimie kuondoa tofauti za kidini na kujenga umoja miongoni mwa Watanzania wa dini zote. Wasipofanya hivyo, wataliingiza taifa katika mgogoro mkubwa ambao hauna msingi kama ilivyotokea katika nchi jirani. Nawaomba wamiliki wa vyombo vya habari kutambua kuwa wanao wajibu wa kuhakikisha vyombo vyao havitumiki kuleta mifarakano kwa kuchochea uhasama baina ya Wakristo na Waislamu.
Hitimisho
Ndugu Wananchi;
Naomba kumaliza kuwa kusisitiza kuwa wananchi wote kudumisha umoja na mshikamano wetu. Tuishi kwa upendo, umoja, mshikamano na ushirikiano bila kujali tofauti ya dini zetu, kabila, rangi au mahali atokako mtu. Hizo ndizo tunu za taifa letu la Tanzania ambazo hatuna budi kuzienzi, kuzilinda na kuzidumisha. Narudia kuwahakikishia kuwa Serikali haipendelei dini yo yote na wala haina mpango wa kushiriki kuangamiza dini yo yote au waumini wao. Serikali kupitia vyombo vyake vya usalama itaendelea kuhakikisha ulinzi na usalama wa raia wake na mali zao kama inavyofanya siku zote. Kama kuna mtu anaona kuwa maisha yake au mali zake zipo hatarini, aende kutoa taarifa Polisi. Hatua zipasazo zitachukuliwa.
Ndugu Wananchi;
Mwisho nawatakia sikukuu njema ya Pasaka. Tusherehekee kwa amani na utulivu. Tusherehekee pamoja.
Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!
Asanteni kwa Kunisikiliza.