Mkurugenzi wa JR & LK Investment, Mchatta Eric Mchatta (katikati) akizungumza na wanahabari, Pembeni ni Wajumbe wa Kamati hiyo, Kudra-Zake Bhukoli (kulia) na Lilian Kitunga (kushoto).
Mjumbe wa Kamati hiyo, Lilian Kitunga (kushoto) akifafanua jambo kwa wanahabari.
---
Na Thehabari.com
KAMPUNI ya JR & LK Investment inatarajia kuzinduwa tuzo yake ya kwanza kwa wasanii wa Muziki wa Asili itakayojulikana kama 'Mwalimu Nyerere Tanzania Contemporary Traditional Muzic Awards'
Tuzo hiyo inatarajia kuwakumbuka wasanii wa nyimbo za asili ambazo ndizo zinazobeba utamaduni wa Mtanzania, ambao umekuwa ukifunikwa na tamaduni za nje kwa muda.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa JR & LK Investment, Mchatta Eric Mchatta alisema kampuni hiyo tayari imepewa kibali na Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) kuendesha tuzo hizo.
Alisema kwa mara ya kwanza tuzo hizo zinatarajiwa kuanzishwa kwenye wiki ya kumbukumbu ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere itakayofanyika kuanzia Oktoba 11, 2013.
Aidha alisema tuzo hizo zina lengo la kuthamini na kuinua kazi za wasanii wa asili, kubadilisha tamaduni na kuheshimu wanamuziki wa asili Tanzania.
"Mwalimu Nyerere katika siku za uhai wake aliwahi kusema; "Taifa bila tamaduni ni sawa na taifa lililo kufa, kwa kuzingatia usemi huo wa Mwalimu Nyerere, JR & LK Investment imedhamiria kwa dhati kuwainua wanamuziki wanao fanya muziki wa asili kwa njia ya kuwashindanisha kwa kupigiwa kura na wananchi...," alisema Mchatta.
Alisema kwa sasa Tanzania imepoteza baadhi ya tamaduni, mila, na desturi zake na badala yake kufuata tamaduni za mabara mengine kama Ulaya na sehemu nyinginezo. "Tuzo za muziki asili za Mwalimu Nyerere zinalenga pia kuwaleta Watanzania wa kila rika, kabila, dini na wanaofanya kazi anuai kuungana na kujifunza uzuri na thamani ya kudumisha tamaduni...," alisema kiongozi huyo.
JR & LK Investment imewaomba Watanzania kukaa mkao wa kuunga mkono tuzo hizo ikiwa ni pamoja na wadau kujitokeza kufanikisha shughuli hiyo inayotarajia kuinua muziki wa asili nchini.