Emerson Oliveira (katikati) na Couthno, wakipokelewa uwanja wa ndege leo mchana.
Mchezaji mpya wa Yanga,Emerson Oliveira Neves Roque (kushoto) akiwasalimia mashabiki wa timu iyo,baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa ndege wa Mwalimu Julius Nyerere na mchezaji mwenzake Andrey Coutinho.
Maximo akiwasili na mchezaji huyo.
---
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.
KIUNGO mkabaji Mbrazil mwenye sifa saba za kiuchezaji, Emerson Oliveira Neves Roque, amewasili jijini Dar es Salaam, leo mchana tayari kufanya majaribio ya kujiunga na klabu ya Yanga SC.
Baada ya kuwasili uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere, akiongozana na Kocha Marcio Maximo na kiungo mshambuliaji Andrey Coutinho, mchezaji huyo alisema; “Ninafurahi kuwafika Tanzania, na niko tayari kupambana, hivyo nimekuja kupambana''.
Akizungumza na waandishi wa habari uwanjani hapo Kocha huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars alisema kuwa Yanga ni timu kubwa yenye wachezaji wengi wenye uwezo mkubwa, hivyo Emerson anatakiwa kupambana.
''Emerson anakuja kuchukua nafasi ya mshambuliaji Genilson Santana Santos ‘Jaja’ aliyejiondoa Yanga kwa matatizo ya kifamilia''. alisema Maximo.
Emerson mwenye umri wa miaka 24 mzaliwa wa Rio de Janeiro, anakuja Yanga SC akitokea klabu ya Bonsucesso ya jijini humo, ambayo imewahi kucheza Ligi ya Serie B mara mbili, ingawa kwa sasa inacheza ligi ya jimbo la Rio de jeneiro.
Mchezaji huyo anatarajiwa kuanza majaribio kesho asubuhi katika mazoezi ya timu hiyo yanayofanyika kwenye viwanja vya Shule ya Sekondari ya Royola.
Jaja alijiunga na Yanga SC msimu huu, lakini hakuwahi kuwavutia wapenzi wa klabu hiyo, ingawa atakumbukwa kwa mabao yake mawili aliyofunga wakati Yanga SC ikiifunga Azam FC 3-0 katika mechi ya Ngao ya Jamii Septemba 14, mwaka huu.
Kwa ujumla, katika mechi 11 Jaja aliifungia mabao sita Yanga SC, moja katika mechi saba za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na matatu katika michezo ya kirafiki mbali na hayo mawili yaliyopeleka Ngao ya Jamii Jangwani.