Mkopo ni makubaliano ya kupeana fedha au vitu kwa lengo la kurudisha fedha/vitu hivyo baada ya muda fulani, kama zilivyo au zikiwa na ziada au riba.
Makubaliano hayo ya mkopo yaweza kufanyika kwa kuhusisha dhamana ya mkopo huo au pasipo dhamana kutegemeana na namna wahusika wenyewe walivyokubaliana.
Makubaliano hayo pia yaweza kuwa ya mdomo au ya maandishi kutegemeana na namna wahusika walivyoona katika kuingia makubaliano hayo.
Mkopo ni moja kati ya nyenzo kubwa sana zinazoweza kutumiwa na mfanyabiashara au mtu yeyote yule, katika kupata pesa zinazoweza kuendesha biashara yake.
Mkopo ukitumiwa vizuri husaidia kuongeza mtaji wa biashara, kukuza wigo wa biashara, kujenga mahusiano mazuri ya kifedha kati ya taasisi ya fedha na kampuni au mfanyabiashara/mjasiriamali.
Huwajengea wafanyabiashara nidhamu ya matumizi bora ya fedha na kujenga mustakabari mzuri wa biashara.
Mambo ya msingi yasipozingatiwa kabla ya kukopa, mkopo huwa ni kero, balaa, mzigo, utumwa na karaha.
Usipokuwa mwangalifu mkopo unaweza kuharibu jina la biashara yako, unaweza kupoteza wateja, kufilisiwa, kupoteza mwelekeo wako kibiashara, kuharibu uhusiano na taasisi za fedha.
Mkopo unaweza kuvunja ndoa, undugu, urafiki na kusambaratisha kabisa uhusiano yaliyodumu kwa muda mrefu kati ya pande mbili.
Kuna umuhimu mkubwa sana wa kuwa makini sana na kuzingatia mambo yote ya msingi kisheria na kibiashara kabla hujakopa.
Kwa mujibu wa Sheria ya Mikataba sura ya 345 kama ilivyorejewa mwaka 2002, ni muhimu sana makubaliano yenu ya mkopo yakawa kwa maandishi, mali iliyokopeshwa ijulikane wazi na kama kuna riba na yenyewe ikawekwa bayana kwenye mkataba na muda maalumu ambayo italipwa.
Kuingia mkataba wa mkopo kwa maneno ni kuhatarisha usalama wa fedha na mali zako. Ni muhimu ijulikane unadaiwa nini, riba kiasi gani, dhamana ni nini, utalipa kwa muda gani, kivipi.
Sheria ya Benki na Taasisi za Fedha sura ya 342 pamoja na kanuni zake inazitaka taasisi za fedha ambazo zinakopesha kuwa na leseni na vibali vyote vya kufanya hivyo.
Ni muhimu ujiridhishe juu ya uhalali wa taasisi hiyo unayotaka kwenda kukopa ili usije ukapoteza kiholela mali zako ulizoweka dhamana.
Kwa mikopo ambayo dhamana yake huwa ni mali ya wanandoa, ni muhimu sana kumshirikisha mwenzi wako kabla ya kufanya chochote. Usimfiche mkeo au mumeo, utakuja kuumbuka mali inapouzwa.
Kama mali ni ya urithi washirikishe warithi wote, usiweke rehani mali ya urithi kimyakimya, utajuta. Usitoe mali yako kienyeji kumdhamini mtu ili akope. Ni muhimu pia kuwa mwangalifu na riba pamoja na masharti ya mkopo unaochukua.
Jiepushe na wajanja wanaokusainisha mkataba wa mauziano wakati hujawauzia mali zako.
Hata kama una vigezo vyote vya kukopa, si vyema ukakopa kama huna maono, mipango wala malengo na fedha hizo. Usikope kama hujui utafanya biashara gani au hujui mkopo huo utaulipaje. Usikope ili kulipa deni, kuoa/kuolewa au kununua vitu ambavyo havitakuingizia pesa. Usikope kununua gari ambalo halitaingiza pesa. Kopa na utumie fedha hizo kwa kununua vitu au kuwekeza katika miradi ambayo itakuingizia fedha. Kopa kwa ajili ya masuala ya maendeleo, siyo anasa.