Meneja wa bia ya Kilimanjaro Premium Lager, George Kavishe akiongea natika uzinduzi wa Mbio za Kilimanjaro uliofanyika jijini Dar es Salaam Novemba 5, 2014 alisema “Sasa tumeingia mwaka wa 13 wa udhamini wa Kilimanjaro Marathon. Tunafurahi kuona Kilimanjaro Marathon kwa mara nyingine tena ikiwa kivutio kwa makampuni mbalimbali, hii ni uthibitisho wa jinsi mbio hizi zilivyoendelea kuwa kubwa na kivutio chini ya udhamini wa Kilimanjaro Premium Lager tangu zilipoanzishwa.”
Mkurugenzi wa Michezo Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bw. Leonard Thadeo akiongea machache wakati wa uzinduzi wa Mbio za Kilimanjaro jijini Dar es Salaam. Pembeni yake ni Meneja wa bia ya Kilimanjaro Premium Lager, Bw. George Kavishe na Meneja Chapa wa Tigo Tanzania Bw. William Mpinga.
Hata sisi tulihudhuria, Kutoka Kulia ni Frank wa Daily News, Mroki Mroki na Mmiliki wa Blog hii Cathbert Angelo.
Mkurugenzi wa Michezo Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bw. Leonard Thadeo akisimika bendera kuashiria uzinduzi wa Mbio za Kilimanjaro jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Michezo Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bw. Leonard Thadeo akiwa na Meneja wa bia ya Kilimanjaro Premium Lager, Bw. George Kavishe.
Picha ya Pamoja ya Wadhamini.
Wageni waalikwa.
Wageni waalikwa wakifuatilia kwa makini.
Burudani kutoka kwa wanafunzi wa Chuo cha Sanaa Bayamoyo.
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.
Mbio za 13 za Kilimanjaro Marathon zinazotarajiwa kufanyika Moshi tarehe 1 Machi, 2015 zimezinduliwa leo jijini Dar es salaam.
George Kavishe, Meneja wa bia ya Kilimanjaro Premium Lager alisema “Sasa tumeingia mwaka wa 13 wa udhamini wa Kilimanjaro Marathon. Tunafurahi kuona Kilimanjaro Marathon kwa mara nyingine tena ikiwa kivutio kwa makampuni mbalimbali, hii ni uthibitisho wa jinsi mbio hizi zilivyoendelea kuwa kubwa na kivutio chini ya udhamini wa Kilimanjaro Premium Lager tangu zilipoanzishwa.”
“Kilimanjaro Premium Lager ina furaha kuona jinsi ambavyo Kilimanjaro Marathon imepata mvuto na kuleta shauku kubwa kwa washiriki wa hapa nchini na wa kimataifa kwa mara nyingine tena mwaka huu. Udhamini wetu kwa Kilimanjaro Marathon umelenga kuwapa nguvu wanariadha wetu na kuendeleza ari ya ushindi ili kuipeleka riadha ya Tanzania juu zaidi.
”Tangu udhamini wetu wa kwanza kwa Kilimanjaro Marathon mwaka 2003, tumeshuhudia ukuaji wa mbio hizi na tuna furaha kubwa kwa fursa ya kuendelea kuwa sehemu ya mbio hizi na kuweza kuwaletea wanariadha wetu tukio kubwa la kimataifa hapa nyumbani. Tunatarajia kuwa na tukio la kusisimua na tunayofuraha kutangaza kwamba Kilimanjaro Marathon 2015 itakuwa ya kuvutia na yenye msisimko zaidi na tunakaribisha watu wote wajitokeze kushiriki mbio hizi za aina yake tarehe 1 Machi 2015.
Akitangaza udhamini wa Tigo kwa mbio hizo, Meneja Chapa waTigo, William Mpinga alisema udhamini huo ni sehemu ya wajibu wa kampuni hiyo katika maendeleo ya michezo nchini na pia katika kusaidia jitihada za uhifadhi wa Mlima Kilimanjaro, kivutio kikubwa cha utalii Tanzania”
“Tuna furaha sana kuwa sehemu ya mbio hizi za aina yake ambazo zimepata mafanikio makubwa sana katika kuutangaza Mlima Kilimanjaro kama kivutio cha kipekee cha utalii hapa nchini na nje.
Kama kampuni ya Kitanzania, tunajivunia mbio hizi kwa kuleta fursa ambayo sio tu uwavutia wanariadha wa kimataifa, lakini pia ni jukwaa muhimu la kuionyesha dunia vipaji vyetu katika riadha,” alisemaMpinga.
Meneja Chapa huyo alisema kwamba mbali na kufurahia mbio za nusu marathon zitakazojulikana kama “Tigo Kili Half Marathon” zinazodhaminiwa naTigo mashabiki na wakazi wa Moshi watapewa fursa ya kujionea bidhaa mbalimbali za dijitali kutoka Tigo na huduma zitakazoonyeshwa kwenye mbio hizo.
Meneja Utawala wa GAPCO, Jumbe Onjero alisema: "GAPCO, wadhamini wa mbio za Marathon za Walemavu kwa kushirikiana na waandaaji Wild Frontiers, Deep Blue Media na Executive Solutions tutatoa msaada wa viti vya magurudumu 50 kwa wahitaji mkoani Kilimanjaro ikiwa ni kuonyesha wajibu wetu kwa jamii.”
Kilimanjaro Marathon ilifanyika kwa mara ya kwanza mwaka 2003 na imekua na kuwa moja kati ya mbio kubwa zaidi barani Afrika ikiwa na washiriki zaidi ya 6,000 kutoka nchi zaidi ya 40.
“Kilimanjaro Marathon imeendelea kuboreshwa kila mwaka, kwenye mbio ya kwanza mwaka 2003 tulikuwa na washiriki 750 tu, lakini kwenye mbio zilizopita tulikuwa na washiriki zaidi ya 6,000 na idadi hii inatarajiwa kuongezeka ukizingatia hizi ndio mbio zenye mvuto zaidi kwa watalii barani Afrika,” alisema John Addison, Mkurugenzi Mkuu wa Wild Frontiers, waandaaji wa mbio hizo.
Mbio hizi zinadhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager (wadhamini wakuu), Tigo (Nusu Marathon), GAPCO (Mbio yaWalemavu), pamoja na wadhamini wa vituo vya maji kwenye mbio hizo ambao ni Kilimanjaro Water, FNB, CMC Automobiles, Simba Cement, TPC Sugar, KK Security, Kibo Palace, na UNFPA.