ALIYEKUWA Mgombea wa Nafasi ya Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka nchini (TFF) kabla ya kuenguliwa na Kamati ya Uchaguzi na ile ya Rufaa, Michael Wambura, amezishukia Kamati hizo pamoja na Katiba nzima inayosababisha utendaji mbovu wa Shirikisho hilo na kuzitaka zitenguwe uamuzi wowote uliosababisha mkanganyiko huo.
Wambura alienguliwa sambamba na aliyekuwa mgombea nafasi ya Urais wa TFF, Jamal Malinzi, ambeya kwa pamoja wameleta mtikisiko mkubwa katika nyanja ya mpira wa miguu hapa nchini, ikiwa ni kuelekea Uchaguzi Mkuu wa TFF uliopangwa kufanyika Februari 24.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo mchana, Wambura alisema Katiba ya TFF inayotumika sasa imepitishwa kimakosa, kutokana na kuamuriwa na mtu mmoja, bila kupigiwa kura na Kamati ya Utendaji ya TFF, sambamba na kukiukwa kwa mambo mengi.
Alisema kuwa Rais wa Shirikisho hilo, Leodgar Tenga, amedanganya umma kwa madai kuwa Katiba inayotumika sasa, baada ya kubadilishwa imepitishwa kihalali, wakati kanuni zake zimeanza kutumika Januari 15, mwaka 2012, wakati Katiba yenyewe imepitishwa Januari 7 mwaka 2013, jambo ambalo linaleta mkanganyiko wa aina yake.
“Haya ndio matatizo yaliyosababisha kuleta mkanganyiko mkubwa, hivyo bila hata kuangalia matokeo yangu, naomba TFF, chini ya Rais Tenga kutengua uamuzi wowote wa Kamati ya Uchaguzi na ile ya Rufaa, pamoja na kutumia Katiba ya zamani, kwasababu waliotoa uamuzi huu wamefanya hivyo kwa sababu ya kuwashughulikia watu wachache, akiwamo Malinzi.
“Katiba ya sasa haijapitishwa kihalali kwakuwa Kamati ya Utendaji haijakutana na kilichopo sasa ni kufanganya tu, huku uamuzi ukifanywa kwa ajili ya kufurahisha upande mmoja, jambo ambalo hakika sitakubaliana nalo hata kidogo,” alisema Wambura.
Akielezea sakata lake la kupeleka mambo ya soka mahakamani, Wambura alisema mwaka 2004, Sunday Kayuni, aliishtaki TFF katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kesi namba 21, lakini leo hii ni Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikisho hilo.
Alisema katika sakata hilo, anashangaa wadau wanaangalia zaidi yeye, jambo ambalo bado hakubaliani nalo na lazima haki itendeke kwa kuvunja uamuzi wowote uliotolewa na Kamati ya Rufaa, kwa madai kuwa imelenga kufanya kazi kirafiki, hasa kwa Mwenyekirti wa Kamati ya Rufaa, Idd Mtinginjola, aliyekuwa swahiba mkubwa wa mgombea wa sasa, Athumani Nyamlani.
Kwa mujibu wa Wam bura, TFF inapaswa kusimamisha matumizi ya Katiba inayotumika kwakuwa sio halali ili kuondoa uwezekano wa kutafutwa haki kwenye Mahakama kiraia, pamoja na kuyafuta maamuzi yoye na kuivunja Kamati ya Rufaa.
Aidha, Wambura alisema kwamba sifa ya mtu kuwa mwenyekiti na Katibu wa Kamati ya Uchaguzi anapaswa kuwa Mwanasheria, jambo ambalo mwenyekiti wa kamati hiyo, Deogratius Lyatto, jambo linaloifanya Kamati hiyo ikose uhalali pamoja na uamuzi wowote unaochukuliwa na watu hao, hiyo ni kwa mujibu wa Ibara ya 49 (4).