Asusa ni kiasi kidogo cha chakula ambacho sio mlo kamili kinachoweza kuliwa bila ya matayarisho makubwa. Mara nyingi huliwa kati ya mlo mmoja na mwingine. Kwa watu wengi hasa wafanyakazi na watoto wa shule ni vigumu kupata milo yote nyumbani na hivyo inabidi wabebe au wanunue kiasi kidogo cha chakula hasa cha asubuhi na mchana. Mara nyingi aina vyakula vinavyopatikana sehemu nyingi ni asusa.
Kwa bahati mbaya asusa zinazopatikana kwa urahisi katika sehemu za biashara ni zile zenye mafuta mengi, sukari nyingi na chumvi nyingi ambazo kiafya sio nzuri. Vilevile mara nyingi mtu anapokuwa na njaa anakuwa na hamu ya kula chakula chochote bila kuchagua. Hivyo unashauriwa yafuatayo:
Chagua asusa zenye virutubisho muhimu
Kuwa mwerevu kwa kuchagua asusa zenye virutubishi muhimu kama matunda, maziwa, juisi halisi ya matunda, karanga, vyakula vilivyochemshwa au kuchomwa kama ndizi, magimbi, viazi vikuu, mihogo, mahindi au viazi vitamu.
Epuka asusua zifuatazo:
-zilizokaangwa au kupikwa kwa mafuta mengi kama sambusa, chips, vitumbua, mihogo, ndizi, na kachori.
-zenye sukari nyingi kama biscut, visheti, kashata, keki, chokoleti, juisi bandia, barafu na soda.
Zenye chumvi nyingi kama krips, bisi zenye chumvi nyingi, soseji nk
Asusa hizi huweza kuchangia kuongezeka uzito wa mwili na uwezekano wa kupata kisukari, shinikizo la damu, baadhi ya saratani na magonjwa ya moyo.
Je ulishaji wa mtoto una uhusiano gani na magonjwa sugu yasioambukizwa?
Tafiti zimeonyesha kuwa kuna uhusiano kati ya ulishaji wa mototo na uwezekano wa kupata magonjwa sugu yasiyoambukizwa utotoni, katika ujana na hata unapokuwa mtu mzima.
Tafiti hizo zimeonyesha kuwa kuwa:
- Unyonyeshaji wa maziwa ya mama huwakinga watoto dhidi ya kuwa na uzito uliozidi na unene uliokithiri wanapokuwa wadogo na hapo badae.
- Watoto walionyonyeshwa maziwa ya mama kwa muda mfupi(chini ya miezi sita) na wale waliopewa maziwa mbadala (maziwa ya kopo au ya wanyama) wako katika hatari zaidi ya kupata baadhi ya magonjwa sugu yasiyoambukizwa kama kisukari, shinikizo kubwa la damu na saratani utotoni katika ujana na wanapokuwa watu wazima.
- Ulishaji wa vyakula vya nyongeza vyenye nishati-lishe kwa wingi unahusishwa na motto kuwa na hatari ya kupata unene saratani na shinikizo kubwa la damu ukubwani.
- Unene wakati wa utoto humuweka mtoto katika hatari ya kupata magonjwa sugu yasiyoambukizwa kama kisukari na ugonjwa wa moyo.
Hivyo mtoto akinyonyeshwa maziwa ya mama pekee kwa miezi sita ya mwanzo na baada ya miezi sita kupewa chakula cha nyongeza kama inavyoshauriwa huku mtoto akiendelea kunyonyeshwa maziwa ya mama mpaka anapotimiza umri wa miaka miwili au zaidi; kuchangia katika kumkinga huyu dhidi ya magonjwa sugu yasiyo ambukizwa ikiwa ni pamoja na utapiamlo ambao pia huweza kuleta madhara mengine utotoni na katika utu uzima. Vile vile, mama anaponyonyesha humpunguzia uwezekano wa kupata saratani ya matimati.
Je, utumie kwa kiasi gani mboga mboga na matunda? Ungana nasi kesho...