Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam.
Kampuni ya simu inayoongoza barani Afrika, Asia na Mashariki ya Kati, Etisalat Group, imeongeza hisa zake katika kampuni ya simu za mkononi ya Zantel kufikia asilimia 85.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Zantel jana jijini Dar es Salaam, hatua hiyo ni ongezeko la hisa hizo kwa asilimia 20 zaidi.
Katika miaka ya hivi karibuni, Zantel imekuwa ikifanya mapinduzi makubwa katika sekta ya simu za mkononi Tanzania kwa ubunifu ambao umekuwa ukisaidia kustawisha maisha ya watu.
Baadhi ya huduma hizo ni pamoja na Z-Kilimo ambayo huwezesha wakulima hata wa vijijini kuweza kupata taarifa muhimu za jinsi ya kuongeza uzalishaji na hivyo kuendeleza sekta ya kilimo.
Huduma nyingine ni Islamic Portal, Discover Tanzania (Tourist Portal) na Reverse Ring Back tone (RRBT) ambazo zinawasaidia watanzania kwa namna mbalimbali.
Pia Zantel ni moja ya kampuni za simu za mkononi nchini zilizofikia makubaliano na kampuni nyingine za simu kuwezesha wateja wao kutuma na kupokea pesa miongoni mwao.
Hii ni huduma ya kwanza ya aina hiyo Afrika ambapo mteja wa kampuni hiyo wa huduma ya EzyPesa anaweza kutuma na kupokea pesa kwenda mitandao mingine.
Kwa sababu ya juhudi zake katika kuokoa maisha ya mama na motto, Zantel imeshawahi kupata tuzo inayoheshimika ya GSMA kwa mradi wa “Mobile Baby”, wakati mkakati wa “Fight Against Malaria” ulitambulika na Wizara ya Afya.