Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Jaji Mkuu Mohamed Chande Othman anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa Bodi mpya ya Baraza la Habari Tanzania (MCT) Agosti 7, mwaka huu katika ukumbi wa Hoteli ya Blue Pearl, jijini Dar es Salaam.
Bodi hiyo ilichaguliwa kwenye Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Wanachama wa MCT uliofanyika Juni 25, 2014 mjini Bagamoyo. Rais mpya wa Baraza ni Mhe Jaji Mstaafu Thomas Mihayo ambaye anachukua nafasi ya Jaji mstaafu, Dr. Robert Kisanga aliyemaliza muda wake. Makamu wa rais wa Baraza ni Bw. Hassan Mittawi ambaye anachukua nafasi ya Bw. Chande Omar Omar ambaye pia amemaliza muda wake. Bwana Mitawi na Bw. Omar ni waandishi nguli wa habari kutoka Zanzibar.
Wajumbe wengine wanaounda Bodi hiyo ni pamoja na Bi Rose Haji, Bi Tuma Abdallah, Bi. Badra Masoud na Bw. Wallace Mauggo ambao wanatoka kwenye tasnia ya habari. Wengine ni Jaji Mstaafu Juston Mlay, Bw. Ali Mufuruki na Prof Bernadetha Killian wanaotoka kwenye kijamii.
Hii itakuwa ni bodi ya sita kuchaguliwa tangu kuundwa kwa Baraza la Habari nchini.
Kabla ya uzinduzi huo, Bodi hiyo mpya itakuwa na kikao chake cha kwanza ambapo pamoja na mambo mengine, itachagua wajumbe wa kamati mbili za Bodi ambazo ni Kamati ya Fedha na Utawala na Kamati ya Maadili.
Katika uzinduzi huo, MCT pia itawaaga wajumbe wa Bodi iliyomaliza muda wake iliyoongozwa na Jaji Kisanga. Wajumbe wengine wa Bodi hiyo iliyomaliza muda wake ni pamoja na Prof.Ruth Meena, Bw. Rafii Haji Makame, Bw. Kenneth Simbaya na Bi. Usu Mallya.
Kajubi D. Mukaganga
Katibu Mtendaji