Mbunge wa Tabora Mjini (CCM) Ismail Aden Rage (wa pili Kulia aliyeshika bomba) akipambana na vijana wa chadema eneo na mti wa kutundika bendera za vyama vyao.
SHEREHE za miaka 36 za kuzaliwa kwa CCM jana ziliingia dosari, baada ya kuibuka vurugu kubwa kati ya wafuasi wa chama hicho na Chadema mkoani Dodoma wakati wakigombea eneo na mti wa kutundika bendera za vyama vyao.
Vurugu hizo zilizotulizwa na Polisi wa Kutuliza Ghasia (FFU), zilitokea jana mchana katika uwanja huo uliopo karibu na Baa ya Mwanga, baada ya CCM kung’oa bendera ya Chadema iliyokuwepo uwanjani hapo, ili waweke bendera zao kwa ajili ya mkutano ambao ulikuwa sehemu ya maadhimisho hayo.
Vurugu zilizuka baada ya wafuasi wa Chadema kuwataka wenzao wa CCM waendelee na mkutano katika eneo hilo kwa sharti la kurejeshwa kwa bendera iliyong’olewa. Wafuasi wa vyama hivyo wakiwamo wabunge wa CCM walionekana wakivutana kunyang’anyana mti wa bendera.