Mkuu wa Shule ya Agape, Rabson Fungo, akiongea katika mahafali hayo.
Wanafunzi wa Kidato cha sita wa Shule ya Sekondari ya Agape, Mbagala, Dar es Salaam, Loveness Hazali (kushoto) na Sophia Mrope, wakiimba moja ya nyimbo za shule hiyo, wakati wa mahafali hayo.
---
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.
Shule ya Sekondari Agape Mbagala imekuwa ya kwanza jijini Dar es Salaam katika matokeo ya kidato cha sita yaliyotangazwa hivi karibuni na kusema nidhamu ya wanafunzi, ushirikiano na kujituma kwa walimu ndiyo siri ya mafanikio.
Mkuu wa shule hiyo, Rabson Fungo, akizungumza na mwandishi wa mtandao huu, alisema shule yake imeshika nafasi ya 15 kwa shule zenye watahiniwa chini ya 30 na kusema ameyapokea matokeo hayo kwa furaha.
Fungo alisema pamoja na shule kuwa na tabia ya kupokea wanafunzi wenye uwezo wa kawaida darasani lakini imejitahidi kuwanoa katika muda wote wanapokuwa shuleni.
Kwa mujibu wa mwalimu huyo, nidhamu ya wanafunzi imerahisisha utekelezaji wa mipango mbalimbali ya kuwaendeleza wanafunzi ikiwemo kufanya mazoezi.
Katika matokeo hayo, wanafunzi wote waliofanya mtihani wa kidato cha sita wataendelea na elimu ya chuo kikuu huku wakati hakuna aliyepata daraja la nne wala sifuri katika matokeo hayo.
Aliwashauri wanafunzi waliopata fursa ya kusoma katika ngazi mbalimbali hapa nchini waitumie vema fursa hiyo ili kuliokoa taifa katika hatari ya kutokuwa na wataalamu siku zijazo.