Habari 2: Karibu watu 108 kati ya wahanga 298 wa ndege ya Malaysia iliyotunguliwa Ukraine Alhamisi walikuwa ni watafiti wa Ukimwi waliokuwa wakielekea Melbourne kuhudhuria Kongamano la 20 la Kimataifa la Ukimwi (AIDS 2014).
AFP imevinukuu vyombo vya habari nchini Australia vikisema kuwa, wakati wa mkutano wa maandalizi ya AIDS 2014 mjini Sidney, washiriki walielezwa kuwa wenzao 100 walikuwa wamepanda hiyo ndege iliyotunguliwa Ukraine Mashariki.
Kati ya waliofariki yumo mtafiti maarufu wa Ukimwi toka Uholanzi, Joep Lange, ambaye amewahi kuwa Rais wa Jumuiya ya Kimataifa ya Ukimwi.
Vilevile, Umoja wa Mataifa umethibitisha kuwa msemaji wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Glenn Thomas, pia amekufa katika mkasa huo.
Malaysian Airlines imetoa orodha ya wahanga inayoonyesha kuwa abiria 189 kati ya 298 walokuwa ndani ya ndege hiyo walitokea Uholazi, huku pia kukiwa na Wamalaysia 44, Waaustralia 27, Waindonesia 12, Waingereza tisa, Wajerumani wanne, Wabelgiji wanne, Wafilipino watatu, Mkanada mmoja na abiria mmoja toka New Zealand.
Utaifa wa abiria wanne waliobaki bado haujafahamika.
Habari 1: Hadi kufikia Ijumaa alfajiri, shirika la ndege la Malaysia limethibitisha abiria 298 wamefariki baada ya ndege yao namba MH17 kutunguliwa Ukraine Mashariki jana.
Kati ya wahanga wa zahama hilo, 150 walikuwa raia wa Uholazi walokuwa wakielekea Kuala Lumpur. Imethibitishwa pia kuwa Waaustralia 27 na Waingereza 9 wamefariki katika shambulizi hilo.
Shirika hilo la ndege limesema litatoa taarifa zaidi litakapokamilisha shughuli ya kuwatafuta ndugu wa marehemu, huku ikitangaza kusitisha safari zake zote Ulaya hadi hapo baadaye.
Wakati huo huo, Marekani pia imeyaonya mashirika yake yanayosafirisha abiria yasithubutu kuruka kwenye anga la Ukraine.
FIRST POST - Kiev, Ukraine. Ndege ya Shirika la Malasyia jana ilitunguliwa mashariki mwa Ukraine na wanajeshi wanaoiunga mkono Russia na kuua watu 295 waliokuwa ndani, ofisa wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Ukraine alisema.
Ndege hiyo ‘Malaysia Airlines’ ilikuwa ikisafiri kutoka Amsterdam kwenda Kuala Lumpur na ilikuwa juu umbali wa futi 33,000 kutoka usawa wa bahari wakati ikitunguliwa.