Lionel Messi ameisaidia Argentina kufika fainali dhidi ya Ujerumani.
NAHODHA wa zamani wa England, David Beckham anatabiri kumuona Lionel Messi akifanya maajabu katika fainali ya kombe la dunia na kuiongoza Argentina kutwaa ubingwa kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1986.
Messi anakosolewa na wadau wa soka kwamba ameshindwa kuonesha kiwango chake cha Barcelona katika soka la kimataifa, lakini amefanya kazi kubwa kuifikisha Argentina katika fainali ya leo usiku dhidi ya Ujerumani.
"Ni mtu wa ajabu," Beckham alisema kwenye mahojiano na chaneli ya Adidas football ya YouTube.
"Anawapa watu presha kubwa kwa aina yake ya uchezaji na kitu kinachompa upekee ni kuweza kucheza kama wenzake, ni mchezaji wa timu".
"Amepata uwezo binafsi mkubwa, lakini ushindi unamaanisha kila kitu kwake. Kama wachezaji wenzake wanafunga mabao, anakuwa wa kwanza kushangilia nao na nadhani ile ina maana kubwa kuhusu yeye"
"Kucheza na Argentina, nina uhakika kuna presha kiasi fulani ukiangalia huko walikotoka. Kushinda ina maana kubwa kwake, familia na kila mmoja anayemzunguka duniani".
Akiwa mgumu kutoa utabiri wake kuhusu mechi ya fainali, Beckham-ambaye atakuwepo kwenye mchezo akiwa na watoto wake, hatimaye aliweka wazi utabiri wake na kusema Argentina itashinda mabao 3-1.
Alisema: "Inashangaza kuwa timu hizi mbili zimekutana pamoja".
"Ujerumani walikuja kwenye michuano wakiwa na uzoefu mkubwa, watu hawajashangaa kuona wamefika hatua hii. Hakuna mchezaji mmoja nyota, wana kundi kubwa la wachezaji wanaocheza pamoja".
David Beckham akimkumbatia Lionel Messi wa Barcelona baada ya mechi ya ligi ya mabingwa.
"Argentina ina kundi la wachezaji wenye vipaji, ambao wanacheza kwa mapenzi makubwa, lakini Lionel, ninafurahia kumuona anacheza."