Na Mohammed Mhina, wa Jeshi la Polisi- Zanzibar
Rais Mstaafu wa Zanzibar Dk. Amani Karume (pichani), amezitaka taasisi za kifedha hapa nchini, kuweka utaratibu wa wazi utakaowanufaisha wananchi wa kipato cha chini ili nao waweze kuchangia katika kukuza uchumi wa taifa.
Dk. Karume ametoa wito huo mjini Zanzibar wakati wa futari iliyoandaliwa na Benki ya NMB kwa wateja wake kisiwani humo, ambapo amesema kukua kwa uchumi wa taifa lolole duniani, kunachangiwa pia na wananchi wa kawaida wanaopata fursa za kushirikishwa katika mifumo ya kiuchumi.
Awali Mkuu wa huduma kwa wateja binafsi Bw. Abdulmajid Nsekela, alisema mbali ya benki hiyokuongeza huduma za kibenki kupitia mitandao ya simu za mkononi, pia imekuwa ikitoa mikopo kwawajasiliamali wadogowadogo wakiwemo waendesha bodaboda na mamalishe.
Amesema kiasi cha shilingi Bilioni 50 za Kitanzania, zimekua zikitumika kwa kila mwezi kwa ajili ya mikopo yenye riba nafuu kwa wateza zaidi ya 5000 wa benki hiyo hapa nchini kwa lengo la kukuza mitaji na kuinua kipato cha mtu mmoja mmoja wa mijini na Vijijini.
Bw. Nsekela, amesema Benki ya NMB , ambayo katika kipindi cha mwaka jana ilipata faida ya zaidi ya shilingi bilioni 132, imepanga kuongeza matawi ya benki hiyo kutoka 152 ya sasa hadi kufikia 170 baadaye mwaka huu kwa lengo na kuwasogezea wateja wake huduma.