Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Saidi Meck Sadiki akizungumza na wajumbe wa kikao cha majumuisho ya ziara ya siku nne ya viongozi na watendaji wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS) iliyofanyika katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es salaam.
Mkiti Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi Dkt. Fatma Mrisho akizungumza na wadau mbalimbali waliohudhuria mkutano wa majumuisho ya hali ya maambukizi mapya ya VVU katika jiji la Dar es salaam mara baada ya kukamilisha ziara ya siku nne mkoani Dar es salaam. Dkt. Fatma ameeleza kuwa maabukizi yameendelea kupungua kutokana na juhudi kubwa inayofanywa na serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.
Naibu Meya wa Manispaa ya Kinondoni Songoro Mnyonge akitoa mchango wake kuhusu namna viongozi wanavyoweza kusaidia kupunguza vitendo hatarishi vinavyochangia maabukizi mapya ya VVU katika maeneo wanayoyaongoza, wakati wa kikao cha majumuisho ya ziara ya siku nne ya viongozi na watendaji wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS) jijini Dar es salaam.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Saidi Meck Sadiki akizungumza jambo na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi Ofisini kwake jijini Dar es salaam.
Wadau mbalimbali waliohudhuria mkutano wa majumuisho ya ziara ya watendaji wa TACAIDS katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es salaam kuangalia hatua iliyofikiwa katika mapambano dhidi ya maambukizi mapya ya VVU katika jiji la Dar es salaam.
Viongozi wa mkoa wa Dar es salaam na Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi wakichukua michango mbalimbali iliyokuwa ikitolewa na wajumbe waliohudhuria kikao cha majumuisho ya ziara ya viongozi wa TACAIDS mkoani Dar es salaam.
Na Na. Aron Msigwa - MAELEZO, Dar es salaam.
Serikali imewataka viongozi na watendaji wa jiji la Dar es salaam kuhakikisha kuwa wanatoa kipaumbele na kuchukua hatua za makusudi kukabiliana na vitendo vyote vinavyochangia maambukizi mapya ya VVU katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es salaam na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Saidi Meck Sadiki wakati wa kikao cha majumuisho ya ziara ya siku nne ya viongozi na watendaji wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS) katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Dar es salaam.
Amesema viongozi na watendaji wa jiji hilo ndio wenye dhamana na jukumu la kusimamia na kuongoza mipango yote ya mapambano ya maambukizi mapya ya VVU wakishirikiana na wananchi katika maeneo wanayoyaongoza na kufafanua kuwa janga la Ukimwi lisipodhibitiwa katika ngazi zote litaendelea kupoteza nguvu kazi na kuiongezea serikali mzigo wa kuwahudumia wagonjwa wapya.
“Nawaagiza viongozi wa manispaa zote tatu za mkoa wa Dar es salaam kulipa kipaumbele kikubwa suala hili la mapambano dhidi ya VVU na Ukimwi kwa kuweka msukumo katika kutoa elimu ili tuweze kuokoa rasilimali zetu” Amesema.
Amesema serikali, vyombo vya habari na Taasisi zilizo kwenye mapambano dhidi ya maambukizi ya VVU zimekuwa zikifanya kazi kubwa ya kutoa elimu ya namna ya kujikinga na janga hili na kuwahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kupima afya zao kwa hiari ili kujua kiwango cha maambukizi ya ugonjwa huo katika maeneo mbalimbali ya jiji.
Ameeleza kuwa licha ya mkoa kukabiliwa na changamoto mbalimbali umeendelea kuchukua hatua za kupunguza maabukizi mapya ya VVU kwa kuweka msisitizo katika utoaji wa elimu, kupiga marufuku ngoma hatarishi za usiku zinazokesha, kutekeleza sheria mbalimbali kupitia jeshi la Polisi ambalo huendesha operesheni mbalimbali za kuwakamata wananchi wanaovunja sheria hususan waendesha biashara za madanguro,watumia madawa ya kulevya na biashara ya ngono kwenye majumba ya starehe.
“Tunaendelea kutoa elimu ya kujikinga na maabukizi mapya ya VVU ili kusaidia hata operesheni mbalimbali tunazofanya katika jiji letu kuzaa matunda na kuwafanya wale wote waliokuwa wakijihusisha na vitendo vinavyochangia kueneza VVU kuachana navyo” Amesisitiza.
Aidha, Bw. Meck Sadiki amegiza kupatiwa orodha ya maeneo yote ya jiji la Dar es salaam ambayo yanaongoza kwa kuwa na vihatarishi vya VVU ili aweze kuyafanyia kazi na kuwaomba wananchi wa mkoa wa Dar es salaam kutoa ushirikiano kwa kuunga mkono juhudi za serikali na kuwafichua wanaoendesha vitendo vinavyochangia maambukizi hayo ili mamlaka husika ziweze kuchukua hatua za kisheria.
Kwa upande wake Mkiti Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi Dkt. Fatma Mrisho akizungumza wakati wa majumuisho hayo amesema kuwa hali ya maambukizi mapya ya VVU katika jiji la Dar es salaam yameendelea kupungua kutokana na juhudi kubwa inayofanywa na serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.
“Ni kweli hali ya maabukizi ya VVU kwa mkoa wa Dar es salaam imeendelea kupungua mwaka hadi mwaka toka asilimia 10.9 mwaka 2004 hadi kufikia asilimia 6.9 za mwaka 2012 jambo linalotufanya tuendelee kuongeza juhudi zaidi ili tufikie malengo ya kitaifa na kimataifa ya kufikia sifuri tatu”. Amesisitiza.
Amesema ili kuhakikisha kuwa vita dhidi ya maambukizi mapya ya VVU inaendelea kufanikiwa , Serikali inashirikiana na taasisi mbalimbali, Baraza na mitandao ya Watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi nchini katika kutoa elimu kwa wananchi kuhusu mbinu za kukabiliana na tatizo hilo.
Ameongeza kuwa serikali inawathamini na inaendelea kuwajengea uwezo Wanaoishi na Virusi vya Ukimwi waliojiunga katika Vikundi vya Kuweka Akiba na Mikopo (VICOBA) katika maeneo mbalimbali nchini kutokana na mwamko mkubwa wa kujiletea maendeleo waliouonyesha.
Ametoa wito kwa WAVIU kote nchini kuendelea kujiunga na mifuko mbalimbali ukiwemo Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ili waweze kunufaika na huduma za afya zinazotolewa kupitia mfuko huo.