Wambura alikwenda mbali zaidi kwa kusema hana haja ya kujadiliwa kwenye mkutano wa Agosti 3, kwa kuwa alishasafishwa kwenye Kamati ya rufaa ya uchaguzi iliyochini ya Mwenyekiti wake Julius Lugaziya.
“Mimi nilishasafishwa kwenye kamati ya Lugaziya na ndio mana nilirudishwa kwenye uchaguzi, na niliondolewa kwa kosa la kufanya kampeni tu hivyo sina haja na mkutano wao,”alisema
Alisema kwa mujibu wa Katiba ya Simba ibara ya 41(d) kuwanyima wanachama fursa ya kujitetea na kusikilizwa kabda ya hatua ni uvunjifu wa haki za msingi za binadamu. Kama zinavyoanishwa kwenye katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 13(6)a pamoja na kanuni za nidhamu za FIFA ibara ya 94(1) na kanuni za adhabu za TFF Ibara ya 35 (1).
Wambura ambaye aliwahi kuwa Katibu wa Chama cha Soka Tanzania (FAT), sasa TFF alisema wanachama waliokwenda mahakamani wana hoja za msingi hivyo wasipuuzwe.
“Wangekuwa hawana hoja hata mahakama kuu isingewapa haki ya kufungua shauri lao, hivyo wasipuuzwe wapewe nafasi ya kusikilizwa,”alisema.
Wambura ambaye hii ni mara ya tano kuenguliwa kwenye uchaguzi alisema kitendo alichofanya Aveva ni cha kidikteta na kitasababisha kuanzisha mtafarakano upya ndani ya klabu hiyo.
Alisema kwa mujibu wa katiba ya Simba Ibara ya 54 (3), uamuzi wowote wa kufukuza wanachama lazima upigiwe kura za siri na wajumbe theluthi mbili waunge mkono, hili japo sio rahisi kama wanavyorifikiria.
“Kuna wakati Hassani Dalali alitaka kumpindua Mwina Kadugunda ila baadae alikwama baada ya wanachama kukataa pendekezo hilo,”alisema.
Alisema uongozi wa Aveva hauwezi kupambana na wanachama zaidi ya 500, hawataweza vita hivi na lazima waingie kwenye migogoro.
Wambura aliishauri uongozi huo utafute suluhisho la mgogoro huo mapema kabda ya mgogoro huo haujawa mkubwa.
Alisema japokuwa hawapewa barua rasmi na Rais wa Simba ila ushauri wake kama wanachama atauwasilisha kwa maandishi kwenye uongozi huo.
“Haya yote nilioongea leo nitayawasilisha kwenye uongozi wa Simba ili wawe na kumbukumbu kama nimeyaongea,”alisema.