Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.
Majambazi wanne jana walilishambulia kwa risasi basi la Jeshi la Magereza lililokuwa limebeba mahabusu baada ya kupora fedha kwenye gari jingine lililokuwa kwenye foleni.
Tukio hilo limetokea siku moja baada ya Kamanda wa Polisi wa Kanda ya Dar es Salaam, Suleiman Kova kutoa taarifa ya kukamata watu wawili wanaodaiwa kuhusika na kifo cha aliyekuwa mtawa wa Kanisa Katoliki, Cresencia Kapuri aliyeuawa Juni 23, eneo la Riverside Ubungo.
Kamanda wa polisi Mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura alisema tukio hilo lilitokea saa 7:50 mchana wakati watu hao walipolifyatulia risasi mbele na nyuma basi hilo lililobeba mahabusu baada ya kupora fedha.
“Gari la Magereza lilikuwa likitokea Kawe likielekea Mahakama ya Kinondoni, ndipo wakaja watu wawili na kushambulia gari hilo kwa risasi mbele na nyuma kisha wakatoweka,” alisema.
“Waliojeruhiwa ni pamoja na dereva wa gari hilo la Magereza, askari wa kike na mahabusu mmoja. Hata hivyo, dereva aliondoa gari kwa kuwa hakujeruhiwa sana, lakini askari wa kike na mtuhumiwa walipelekwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa ajili ya matibabu. Hakuna mahabusu aliyekimbia.”
Hata hivyo, Wambura hakutaja majina ya askari hao wala mtuhumiwa akisema kuwa yalikuwa mbali kwa wakati huo.
Kwa mujibu mashuhuda wa tukio hilo, watu wanne walifika katika eneo la Msasani kwa Mwalimu Nyerere karibu na Hoteli ya Regency wakiwa na pikipiki mbili.
“Walipofika hapa wawili waliokuwa na bunduki walishuka na kwenda kwenye gari dogo jeusi aina ya Range Rover na kuanza kuligonga huku wakidai pesa,” alisema shuhuda aliyejitambulisha kwa jina la Msuya.
“Mmoja alikuwa nyuma na mwingine alikuwa kwenye mlango wa dereva. Kuna wakati dereva alifungua dirisha na kulifunga.
Walipoendelea kugonga dereva wa ile gari alifungua dirisha na kutupa bulungutu la fedha. Walilichukua na kurudi kwenye pikipiki zao.”
“Wakati wanaondoka, mmoja wa waliokuwa na bunduki akakutana na gari la Magereza, akalirushia risasi kwa mbele na kupiga tena kwa nyuma kisha akakimbia kwenye pikipiki na wakatoweka,” alisema shuhuda huyo.